Maombolezo ya Kifo cha Papa Francisko: Wahudumu wa Makanisa Makuu Roma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
“Sacrum novendiale, Novendia” ni kipindi cha siku tisa za maombolezo kinachofuatia kifo cha Baba Mtakatifu na kuanza mara baada ya mazishi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na tarehe yake hupangwa na Baraza la Makardinali na maadhimisho haya yanafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican, Dominika tarehe 27 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya pili ya Novendia, maalum kwa wafanyakazi pamoja na raia wanaoishi mjini Vatican. Kardinali Parolin katika mahubiri yake amegusia kuhusu: Majonzi makubwa katika kipindi hiki cha maombolezo ya Baba Mtakatifu Francisko, lakini jambo la msingi ni furaha ya Pasaka; changamoto mamboleo katika maisha ya vijana, lakini wanapaswa kujikita katika upendo ambao hustahimili yote. Upendo wenye huruma ni kiini cha mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo na kwamba, Kanisa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu.
Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, Jumatatu jioni tarehe 28 Aprili 2025 akiwa ameungana na waamini wa Jimbo kuu la Roma, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya Tatu ya Novendia. Katika mahubiri yake amegusia majonzi makubwa kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma ambao wanaomboleza kwa kuondokewa na Mchungaji wao mkuu, sasa wamekuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, huyu ni mchungaji aliyewapenda sana kondoo wake, lakini wakumbuke kwamba, Kristo Yesu ndiye mchungaji wa kweli, aliyeleta mageuzi katika historia ya ukombozi wa mwanadamu, anatambua uzito wa mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu. Kipindi hiki cha majonzi ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kwani maisha yana nguvu zaidi ya kifo.
Kardinali Mauro Gambetti, O.F.M. Conv., Makamu Askofu mjini Vatican, akiwa ameungana na wahudumu wa Makanisa makuu Jimbo kuu la Roma, Jumanne jioni tarehe 29 Aprili 2025 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Katika mahubiri yake, Kardinali Gambetti anasema, Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, toka huko, Kristo Yesu atakuja kuwahukumu wazima na wafu na Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Yeye ni Bwana wa ulimwengu na wa historia. Ndani yake historia ya mwanadamu na pia kazi nzima ya uumbaji hujumlishwa na kutimilizwa kwa namna iliyo bora kabisa. Ukombozi ni chemchemi ya mamlaka ya Kristo Yesu ambayo anayatekeleza kwa nguvu ya Roho Mtakatifu juu ya Kanisa. Manabii na hatimaye, Yohane Mbatizaji alitangaza katika mafundisho yake kuhusu hukumu ya siku ya mwisho. Hapo matendo ya kila mmoja yatafunuliwa pamoja na siri za nyoyo za watu. Kumbe, huu ni wakati muafaka wa kutumia vyema neema ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo kwani hiki ndicho kitakachokuwa ni kipimo Siku ya hukumu ya mwisho.
Anasema, matendo ya huruma kiroho ambayo kimsingi ni ushauri kwa wenye shaka, kuwafundisha wajinga, kuwaonya wakosefu; kuwafariji wenye huzuni; kusamehe makosa; kuvumilia wasumbufu pamoja na kuwaombea walio hai na wafu ni fursa ya kuwa karibu na wale wanaojisikia kuwa mbali na Kanisa au kusukumizwa pembezoni mwa maisha na utume wa Kanisa! Matendo ya huruma kimwili ni: Kuwalisha wenye njaa; Kuwanywesha wenye kiu; Kuwavika wasio na nguo, Kuwakaribisha wasio na makazi; Kuwatembelea wagonjwa; Kuwatembelea wafungwa pamoja na Kuwazika wafu. Lengo la matendo ya huruma kiroho na kimwili ni kuwawezesha waamini kushiriki katika furaha ya Bwana wao, katika Ufalme wa Mbinguni, kwani Kristo Yesu aliyezaliwa kwake Bikira Maria kwa njiaya Roho Mtakatifu, katika maisha yake ya hadhara aliweza kushiriki mambo yote ya kibinadamu, isipokuwa hakutenda dhambi, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu na kwamba, hiki ni kielelezo cha upendo, huruma na mshikamano wake na watu waaminifu wa Mungu.
Mama Kanisa amempoteza Baba Mtakatifu Francisko; kiongozi aliyependa, aliyeteseka na waja wake, aliyesali na kuombea amani; aliyependa kuwakumbatia na kuwaambata watu wote wa Mungu; alionesha upendo wake usiokuwa na kifani; mtu mwenye hekima na busara; shuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na kwa hakika alikuwa ni mtu wa amani. Kumbe, watu wote wanakaribishwa ili kuishi ndani ya Kanisa kwa sababu: “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.” Mdo 10: 34-35. Ushuhuda wa upendo ndiyo nyenzo muhimu sana ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na wala si wongofu wa shuruti. Kumbe, kuna haja kwa waamini kutangaza na kushuhudia imani tendaji inayopata chimbuko lake katika kiri ya imani, taaalimungu sanjari na Sakramenti za Kanisa.