Tafuta

Upendo wenye huruma ni kiini cha mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo Upendo wenye huruma ni kiini cha mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo   (ANSA)

Mazishi ya Papa Francisko Kielelezo cha Umoja, Mshikamano na Udugu wa Kibinadamu!

Ibada na hatimaye maziko ya Papa Francisko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Roma, limewagusa na kuwashirikisha watu kutoka katika medani mbalimbali za maisha, waamini na wasiokuwa na dini; marafiki, lakini hawakukosekana pia maadui wake. Watu wote hawa walikuja kusikiliza maneno ya Mtakatifu Petro “akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda hakubaliwa na yeye."

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia ambaye pia “Camerlengo” mkuu wa Kanisa Katoliki. Huyu ni kiongozi mkuu wa shughuli za Kanisa wakati kunapotokea kwamba, Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro kiko wazi kwa sababu mbalimbali. Jumatatu ya Pasaka, tarehe 21 Aprili 2025 alitangaza kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha Baba Mtakatifu Francisko, aliyekuwa na umri wa miaka 88 kilichotokea Jumatatu tarehe 21 Aprili 2025 majira ya Saa 1:35 Asubuhi kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 2:35 Asubuhi kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Katika tamko lake, alisema, Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika maisha na utume wake amewafundisha watu wa Mungu umuhimu wa kutangaza na kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili kwa uaminifu, ujasiri na upendo kwa wote, upendeleo wa pekee ikiwa ni kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Mama Kanisa anamshukuru sana Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa ushuhuda na mfano wa maisha yake kama mfuasi wa Kristo Yesu, Kanisa linapenda kuiweka roho ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwenye huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Mazishi ya Papa Francisko limewagusa watu kutoka medani mbalimbali
Mazishi ya Papa Francisko limewagusa watu kutoka medani mbalimbali   (ANSA)

Ni katika muktadha huu, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025 amewaongoza watu wa Mungu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko pumziko la amani, furaha na maisha ya uzima wa milele, nyumbabni kwa Baba wa milele, ambako furaha yake haina mwisho. Kardinali Giovanni Battista Re, katika mahubiri yake kwa ufupi kabisa alitoa muhtasari wa maisha na utume wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko, kama shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu na hasa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Alisimama kidete kuragibisha umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwani uharibifu wa mazingira ni chanzo cha umaskini mkubwa. Baba Mtakatifu Francisko alikazia ujenzi wa udugu na urafiki wa kijamii ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utunzaji bora wa mazingira. Kimsingi vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu wote, kumbe kuna haja ya kujenga na kudumisha mchakato wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutabisha watu wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Papa Francisko ni Baba wa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
Papa Francisko ni Baba wa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni   (ANSA)

Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Dr. Paolo Ruffini, anasema, Ibada na hatimaye maziko ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma, limewagusa na kuwashirikisha watu kutoka katika medani mbalimbali za maisha, waamini na wasiokuwa na dini; marafiki wa Baba Mtakatifu, lakini hawakukosekana pia maadui wake. Watu wote hawa walikuja kusikiliza maneno ya Mtakatifu Petro “akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.” Mdo 10: 34-35.

Makardinali wakisindikiza Jeneza la Papa Francisko
Makardinali wakisindikiza Jeneza la Papa Francisko   (ANSA)

Watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamefika mjini Roma kushuhudia imani, matumaini na mapendo, yaliyotangazwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko enzi ya uhai wake, changamoto ni kuhakikisha kwamba, wanakuwa tayari kujikita katika ujenzi wa ulimwengu mpya unaosimikwa katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano. Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ulisheheni umati mkubwa wa vijana wenye umri wa miaka ishirini wanaoshiriki katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo; Wakleri walioshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kielelezo cha imani tendaji. Maboresho ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii, yameliwezesha tukio la Ibada ya Misa Takatifu na hatimaye mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko kuweza kushuhudiwa na umati mkubwa wa watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Kaburi la Baba Mtakatifu Francisko Kanisa Kuu la B.Maria Mkuu
Kaburi la Baba Mtakatifu Francisko Kanisa Kuu la B.Maria Mkuu   (ANSA)

Mama Kanisa anakiri na kufundisha juu ya “Ufufuko wa wafu na uzima wa milele.” Kumbukumbu ya Waamini Marehemu kwa upande mmoja inagubikwa na huzuni na kwamba, makaburini ni mahali ambapo panaonesha huzuni ya moyo. Ni mahali ambapo waamini wanawakumbuka na kuwaombea ndugu, jamaa na marafiki zao waliotangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Makaburi yanawakumbusha waamini kwamba, hapa duniani wao ni wasafiri na wala hawana makazi ya kudumu. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, kumbukumbu ya waamini Marehemu ni tukio la matumaini katika ufufuko wa wafu, ndiyo maana waamini wanaendelea kuyapamba makaburi kwa maua. Ni kumbukumbu ambayo imechanganyika kati ya huzuni na matumaini; mambo msingi yanayogubika nyoyo za waamini wanapowakumbuka na kuwaombea Marehemu wao. Matumaini ya ufufuko wa wafu yanawasaidia waamini kuendelea na hija kuelekea katika Fumbo la kifo, hapa kila mtu anashiriki “kivyake vyake.” Kuna baadhi watakabiliana na Fumbo la kifo kwa mateso na mahangaiko makubwa, lakini daima wakiwa na maua ya matumaini ya ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Imani kwamba kuna maisha baada ya kifo ni ya kale kabla hata ukristo haufika!

Shuhuda wa Huruma
27 Aprili 2025, 14:47