Mazishi ya Papa Francisko: Muhtasari wa Maisha na Utume Wake!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maelfu ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia wameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, Ibada iliyoongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali. Mara baada ya Misa Takatifu, maandamano yalianza kutoka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Njiani watu walijipanga kutoa salam zao za mwisho kwa Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anapelekwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, ili kupumzishwa kwenye usingizi wa amani, Ibada ambayo imeadhimishwa kwa faragha na Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia ambaye pia “Camerlengo” mkuu wa Kanisa Katoliki. Huyu ni kiongozi mkuu wa shughuli za Kanisa wakati kunapotokea kwamba, Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro kiko wazi kwa sababu mbalimbali. Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ameliangazia Fumbo la Mateso na Kifo cha binadamu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yake, hasa pale, watu wanapoondokewa na wapendwa wao! Hata Kristo Yesu, mbele ya kaburi la rafiki yake Lazaro alitoa machozi, ushuhuda kwamba, Yesu yuko karibu sana na waja wake kama ndugu! Kwa uchungu mkubwa alimwombea Lazaro kwa Baba yake wa mbinguni, chemchemi ya uhai na hatimaye, akamwamuru Lazaro aliyekufa kutoka nje ya kaburi! Huu ndio mwelekeo wa matumaini ya Kikristo katika kukabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu “anasimama dede” kupambana na kifo ambacho kimejitokeza katika kazi ya uumbaji kinyume kabisa cha upendo wa Mungu na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu ambaye ameganga na kuponya Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu. Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima.” Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini. Mbele ya Fumbo la Kifo binadamu ni mnyonge na ni “mdogo sana kama kidonge cha piliton”. Lakini, neema katika hali na mazingira kama haya, inaweza tena kuamsha imani na Yesu mwenyewe kuwashika mkono watu wake na kuwaambia “Talitha kum” tafsiri yake “Msichana, nakuambia, inuka.” Haya ni maneno ambayo Yesu anapenda kumwambia kila mtu, simama na fufuka tena! Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ndiyo matumaini ya Kikristo mbele ya Fumbo la Kifo. Kwa mwamini hili ni lango ambalo liko wazi; lakini kwa mwenye mashaka, ni giza linalomwandama na kumtumbukiza mtu katika majonzi na msiba mkuu. Kwa kila mwamini, hii itakuwa ni neema siku ile mwanga huu utakapoangaza.
Kardinali Kevin Joseph Farrell, Jumatatu ya Pasaka, tarehe 21 Aprili 2025 alitangaza kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha Baba Mtakatifu Francisko, aliyekuwa na umri wa miaka 88 kilichotokea Jumatatu tarehe 21 Aprili 2025 majira ya Saa 1:35 Asubuhi kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 2:35 Asubuhi kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Katika tamko lake, alisema, Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika maisha na utume wake amewafundisha watu wa Mungu umuhimu wa kutangaza na kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili kwa uaminifu, ujasiri na upendo kwa wote, upendeleo wa pekee ikiwa ni kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Mama Kanisa anamshukuru sana Baba Mtakatifu Francisko kwa ushuhuda na mfano wa maisha yake kama mfuasi wa Kristo Yesu, Kanisa linapenda kuiweka roho ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwenye huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni katika muktadha huu, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025 amewaongoza watu wa Mungu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko pumziko la amani, furaha na maisha ya uzima wa milele, nyumbabni kwa Baba wa milele, ambako furaha yake haina mwisho. Kardinali Giovanni Battista Re, katika mahubiri yake, ametambua uwepo wa wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliofika mjini Vatican ili kutoa heshima zao kwa Hayati Baba Mtakatifu Francisko, bila kuwasahau wale wote ambao wameguswa na kutikiswa na msiba huu mzito. Licha ya changamoto kubwa ya ugonjwa aliyokuwa anakabiliana nayo, Hayati Baba Mtakatifu Francisko hakusita kutoa Salam na Baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2025 na baadaye akateremka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kusalimiana na mahuaji wa matumaini waliokuwa wamefurika uwanjani hapo.
Mama Kanisa anasali ili kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo aweze kumwangazia Baba Mtakatifu Francisko mwanga na utukufu wa Baba wa milele uliosheheni huruma na upendo. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alimkabidhi Mtakatifu Petro dhamana ya kuliongoza Kanisa lake, kuwalisha kondoo wake na kutoa huduma ya upendo, huku akifuata nyayo za Kristo Yesu: “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Mk 10:45. Hayati Baba Mtakatifu Francisko amejitahidi kumfuasa Kristo Yesu, akajisadaka bila ya kujibakiza, katika hali ya amani na utulivu wa ndani, akionesha ukaribu wake kwa watu wa Mungu huku akitambua kwamba, “Ni heri kutoa kuliko kupokea.” Mdo 20:35. Hayati Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Machi 2013 alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, alikuwa tayari amekwisha “kuonja chumvi nyingi ya maisha ya kitawa kama Myesuit, na miaka 21 ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo kuu la Buenos Aires kama Askofu Msaidizi, Askofu mkuu mwandamizi na hatimaye kama Askofu mkuu. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko akasimikwa rasmi na kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi na kutoa kipaumbele cha pekee kwa: Maskini, Amani, Mazingira na Ujenzi wa Udugu wa kibinadamu. Akaonesha kuwa ni mtu wa watu kwa ajili ya watu wa Mungu, akaonesha moyo wazi kwa kila mtu, lakini upendeleo wa pekee wakiwa ni maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, huku akitoa mwaliko kwa watu wa Mungu kushughulikia changamoto mambo leo kwa mwanga wa tunu msingi za Kiinjili, huku wakiendelea kumsikiliza Roho Mtakatifu. Ni kiongozi aliyeonja uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi, furaha na matumaini ya watu wa Mungu, akawa kweli ni chombo na shuhuda wa ukarimu, akajenga utamaduni wa kusikiliza pamoja na kuwatia moyo wale wote waliovunjika na kupondeka moyo; akajitahidi kuamsha tena kati ya watu kanuni maadili na utu wema sanjari na maisha ya kiroho.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko alitoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; hii ni furaha ya Injili “Evangelii gaudium” inayofumbatwa katika imani, matumaini na mapendo kwa kujiamimisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu. Alipenda kuyaona malango ya Kanisa yakiwa wazi, Kanisa kama Hospitali kwenye uwanja wa vita; Kanisa lenye uwezo wa kuinama, kugusa na kuganga madonda ya watu wa Mungu kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Hawa ni maskini, wakimbizi na wahamiaji, wakawa ni watu wa kwanza kutembelewa naye kule Lampedusa, Lesbo na wakati wa hija yake ya Kitume nchini Marekani. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, amefanya hija za kitume 47 sehemu mbalimbali za dunia. Lakini hija ya kitume ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 ilinogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hii ni hija iliyofumbata mambo makuu matatu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa Wakristo nchini Iraq, uhamasishaji wa ujenzi wa Iraq mpya katika haki na usawa na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu alikuwa nchini Iraq kama hujaji wa toba, ili kumwomba Mungu msamaha na kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa. Alikuwa kati pamoja nao kama hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Anapenda kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini. Hii ni hija iliyokazia pia umuhimu wa majadiliano ya kiekumene. Kuna mwako 2024 Baba Mtakatifu Francisko alifanya hija ya kitume kwa kutembea Mataifa yaliyoko Oceania, pembezoni mwa dunia.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Injili ya Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke hasi na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Huruma ya Mungu anaendelea kusema Baba Mtakatifu Francisko inawasha moto wa upendo mioyoni mwa watu, kwa kuguswa na mahitaji yao pamoja na kuwashirikisha. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuishi kwa furaha yote haya. Huruma ya Mungu na furaha ya Injili ni mambo msingi katika maisha na utume wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni chombo madhubuti katika kukuza na kudumisha mchakato wa utamaduni wa majadiliano, amani, haki jamii na udugu wa kibinadamu. Waraka unaonesha umuhimu wa dini kulinda, kutunza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa wote. Ni wajibu wa dini kudumisha, haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Waamini wa dini mbalimbali washikamane na kutembea kwa pamoja, kwa sababu tofauti zao msingi ni mpango wa Mungu, amana na utajiri unaopaswa kuendelezwa. Majadiliano ya kidini yageuzwe kuwa ni sehemu ya sala inayowaunganisha na kuwafanya kuwa ndugu wamoja.
Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anajikita katika mambo yanayoendelea kujiri katika mazingira; Injili ya Kazi ya Uumbaji na Amani Duniani; Vyanzo vya mgogoro wa Ikolojia na jinsi vinavyohusiana na watu; Ikolojia ya mazingira, uchumi na jamii. Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni kuhusu umuhimu wa elimu ya ikolojia inayojikita katika wongofu wa ndani, furaha na amani, Sakramenti za Kanisa pamoja na sala. Waraka huu una mwelekeo wa umoja na mshikamano ambao unadhihirishwa na mchango uliotolewa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema ni wajibu wa kimaadili na kiutu ili kuwasha moto wa: haki amani; Upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kurejea tena kwa ari na nguvu mpya katika majadiliano yanayofumbata ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vita hii ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu wote. Kuna haja ya kushinda kishawishi cha kukimbilia mapambano ya silaha kama njia ya kutatua migogoro ya Jumuiya ya Kimataifa. Kimsingi vita ni uwanja wa vifo na maafa makubwa kwa watu na mali zao.
Mtakatifu Francisko katika Waraka huu, anapembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa na kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote! Kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu. Wakristo wote wanaungana ili kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kumpokea katika huruma na upendo wake usiokuwa na mwisho, na kamwe waamini na watu wote wenye mapenzi mema wasisite kuendelea kumwombea, Hayati Baba Mtakatifu Francisko, ili huko mbinguni aendelee kuwabari watu wa Mungu, wanaotafuta ukweli huku wakiendelea kuwasha moto wa matumaini.