Mazishi ya Papa Francisko
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Ni Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025 ambapo Misa ya mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko ikiwa inakaribia kuanza na kutangazwa na vyombo vya habari Ulimwenguni kote kwa kuongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali ilisikika sauti ya kengele ya kifo.
Kwa wakonselebranti karibia 5,000 wakiwemo makardinali, maaskofu, mapadre na mashemasi wanaonekana katika Uwanja wa Mtakatifu Petro. Wanashiri kwa hiyo wawakilishi kutoka watawala, kutoka makanisa ya kiekumene na dini nyingine mbali mbali za dunia, waamini wote wenye mapenzi mema kuanzia uwanja wa Mtakatifu Petro hadi mwisho wa njia ya Conciliazione!
Rangi kuu katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro inayotawala ni nyekundu ya makardinali, ambao, wameingia kwa maandamano, huku wakichukua nafasi zao upande wa kushoto wakitazama Basilika, pamoja na maaskofu ndugu zao na nguo nyeusi za wawakilishi karibu 170, kutoka duniani kote wanaowakilisha nchi zao katika safu tofauti kwa upande wa kulia wa uwanja wa Mtakatifu Petro.
Jeneza lenye mwili wa Papa Bergoglio, lilibebwa kutoka katikati ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro wakati pembeni, kulikuwa na mistari miwili ya makardinali pande mbili, jeneza likapita katikati yao. Muda mfupi kabla, katika Basilika hiyo heshima za wakuu wa nchi ziliendelea ikiwa ni pamoja na rais wa Ufaransa Macron na mkewe Brigitte, William wa Uingereza na Albert wa Monaco, mfalme na malkia wa Jordan, Trump na mkewe Melania, Matarella na mtoto wake wa kike, Zelensky na wengine wengi walitoa heshima zao chini ya Madhabahu ya Kukiri, ambapo mwili wa Papa aliyekufa tangu tarehe 23 Aprili ulibaki kwa siku tatu na kuruhusu waamini wenye mapenzi mema kutoa heshima zao wakati jeneza likiwa wazi. Kwa takwimu iliyotolewa kuhusu heshima hizo, waamini karibu 250,000 walitoa heshima zao.
[ Photo Embed: Wakuu wa chini na serekali mbali mbali ]
Mara tu jeneza lenye mwili wa Papa Francisko lilipotokea uwanjani, yalisikia makofi ya kishindo kutoka kwa mamia ya maelfu ya waamini waliokuwepo, huku umati ukiwa umefurika hadi njia ya Conciliazione.
Juu ya jeneza, kama ilivyo desturi katika mazishi ya papa, iliwekwa Injili iliyofunguliwa wazi.