Mazishi ya Papa Francisko,Kard Re:'Jengeni madaraja na siyo kuta'
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Uwanja wa Mtakatifu Petro umekumbatia kwa mara ya mwisho mpendwa sana Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025. Katika misa iliyoongozwa na Dekano wa Baraza la Makardinali Giovanni Bastisti Re, alisisitiza sifa za Ubaba wa Upapa wake katika mahubiri ambapo alimfafanua Baba Mtakatifu kuwa aligusa "akili na mioyo ya wengi na alikuwa na sura yake hiyo itabaki mioyoni mwetu. Alikuwa na utu imara katika uongozi wa Kanisa na alikuwa Papa kati ya watu mwenye moyo wazi kwa wote.
Kwake yeye Kanisa ni makao ya wote na alikuwa na ishara nyingi za kuwapendelea masikini, wakimbizi na watu waliohamishwa. Huruma na furaha ni maneno mawili muhimu ambayo alikazia katika upapa wake na wakati huo umuhimu wa udugu ulienea katika upapa nzima. Papa Francisko alipaza sauti yake kwa ajili ya amani bila kukoma na kusisitiza kujenga madaraja na siyo kuta. Kabla ya kifo chake alitoa Baraka kwa Kanisa la Roma na ulimwengu na zaidi kwa wanadamu wanaotafuta ukweli.
Kardinali Re kwa kuhitimisha mahubiri yake alisema "Sasa, Baba Mtakatifu Francisko, tunakuomba utuombee na tunakuomba kutoka mbinguni ubariki Kanisa, ubariki Roma ubariki ulimwengu wote, kama ulivyofanya Dominika iliyopita kutoka kwenye balcony ya Kanisa hili katika kumbatio la mwisho kwa watu wote wa Mungu, lakini pia kwa wanadamu wote, kwa ubinadamu unaotafuta ukweli kwa moyo wa kweli na kuinua mwanga wa matumaini."
Baada ya litania, Kardinali Baldassarre Reina, Makamu wa Papa jimbo la Roma, aliongoza maombi ya Kanisa la Roma. Kisha mapatriaki wa kiorthodox, maaskofu wakuu na wakuu wa Makanisa ya Miji mikuu ya Mashariki ya Kikatoliki walioko kwenye kanuni ya "sui iuris" walikuja mbele ya jeneza kwa ajili ya maombi ya Makanisa ya Mashariki wakati nyimbo zao za kiutamaduni zikiimbwa.
Hata wakati wa mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko, kama ilivyokuwa miaka ishirini iliyopita wakati wa mazishi ya Papa Yohane Paulo II, upepo ulifungua na kufanya kurasa za Injili zionekane zikifunguka, juu ya jeneza kugeuka. Haya yote yalitokea katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mara moja kabla na wakati wa kunyunyiza maji na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali na pia kufukia uvumba utolewa katika ibada ya mazishi.
Kwa hiyo mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko yalimalizika, huku kukiwa na shangwe za umati wa watu wakisindikiza Jeneza kurejeshwa Kanisa kuu likisindikizwa na msafara wa makardinali, hadi kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kabla ya kuanza msafara wa mazishi kwa mwendo wa taratibu kuelekea Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu, mahali pa kuzikwa kwa faragha.
Bila kupita kwenye uwanja, Jeneza likiwa kwenye kigari cha Kipapa lilielekea kwenda Basilika ya Mtakatifu Maria ambapo waamini walionekana kusimama nyuma ya vizuizi vilivyowekwa barabarani katika siku ambayo Mungu amependa kutoa joto la jua lenye kupendeza na anga la bluu safi na mawingu meupe.
kila kundi watu walisema “viva il Papa.” Kwa mujibu wa taarifa za mwisho, zaidi ya waamini 250,000 walishiriki misa ya mazishi. Pamoja na Ultima Commendatio (pendekezo la mwisho) na Valedictio (kuaga), ibada ya mazishi ya Papa Francisko ilifikia hatua yake ya mwisho, ikifuatiwa na mamia ya maelfu ya watu ambao, katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na kando ya Njia ya Conciliazione hadi Uwanja wa Pia tulipo sisi Baraza la Kipapa la Mawasiliano, walitoa heshima zao za mwisho kwa Papa wa kwanza wa Argentina katika historia ya Kanisa.