Mchakato wa Uchaguzi wa Papa Mpya Utaanza Tarehe 7 Mei 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wakati ambapo kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kinapokuwa wazi, shughuli msingi za Kanisa zinaendeshwa na Baraza la Makardinali, lakini kwa maneno machache ni shughuli zinazoendeshwa mintarafu Sheria na kanuni za Kanisa. Katika kipindi hiki, Mabaraza ya Kipapa yanawajibika kutekeleza majukumu yake ya kawaida, kwani kimsingi anapofariki dunia Khalifa wa Mtakatifu Petro kama ilivyokuwa kwa Baba Mtakatifu Francisko, Marais na Wenyeviti wa Mabaraza ya Kipapa nyadhifa zao zinakoma kisheria, kwani kadiri ya sheria za Kanisa wanakosa rejea na maamuzi ya mwisho yanayopaswa kutolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. “Con-clave”: neno ambalo litasikika sana wakati huu wa mchakato wa kumchagua Papa Mpya linatoholewa kutoka katika Lugha ya Kilatini, maana yake, “Kufunga na ufunguo.”
Wakati wa uchaguzi wa Papa Mpya, Makardinali wenye dhamana ya kupiga na kupigiwa kura hujifungia kwenye Kikanisa cha Sistina kilichoko mjini Vatican. Hiki ni kile kipindi kilichokubalika katika kukuza na kuimarisha misingi ya imani, matumaini na mapendo ya kidugu miongoni mwa Familia ya Mungu; lakini kwa namna ya pekee kwa Makardinali waliokabidhiwa dhamana ya kushiriki katika mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo makini cha imani, matumaini, mapendo, umoja na mshikamano wa Kanisa. Baraza la Makardinali, katika mkutano wao wa tano, Jumatatu tarehe 28 Aprili 2025 limeamua kwamba, mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro uanze rasmi Jumatano tarehe 7 Mei 2025. Kuna jumla ya Makardinali 135 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura, lakini wanaoshiriki ni 133. Muda wa kumaliza uchaguzi huu, bado unaendelea kubaki kitendawili. Waamini wanaalikwa kufunga na kusali, ili kuwasindikiza Makardinali katika tukio hili lenye umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Makardinali wanaendelea kujadili maisha na utume wa Kanisa; mchakato wa uinjilishaji; Majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Makardinali pia wametoa wasifu kwa ajili ya Papa mpya, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kuliandama Kanisa.
Uchaguzi wa Baba Mtakatifu kwa wakati huu unafanyika katikati ya Maadhimisho Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” Waamini wanakumbushwa kwamba, hata kama Baba Mtakatifu Francisko amefariki dunia, lakini Kristo Yesu bado anaendelea kuliongoza Kanisa lake kwa njia ya Roho Mtakatifu na kamwe haliwezi kuwa ni yatima! Ni mwaliko kwa waamini kuyaangalia matukio yote haya kwa jicho la imani na matumaini mintarafu mpango wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Hapa neno Conclave, yaani “Con Chiave” kwa lugha ya Kiitalia; Waswahili wakatafsiri kwa kusema “kufunga na ufunguo” linapata umuhimu wa pekee. Ni Makardinali peke yao wanaoruhusiwa kuhudhuria mikutano hii kwani hapa wanalichambua Kanisa “kama karanga” ili kubainisha hali ya Kanisa, matatizo yaliyopo, fursa na changamoto ambazo wanapaswa kuzifanyia kazi kwa siku za usoni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa. Kutokana na mwelekeo kama huu, hapa Makardinali wanaanza kupata walau “fununu” ya Papa anayetarajiwa na Mama Kanisa. "Conclave," neno ambalo tutaendelea kulitumia jinsi lilivyo ni kipindi cha sala. Ndiyo maana Makardinali kila siku jioni wanakutanika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kusali, kutafakari na kuabudu Ekaristi Takatifu. Sehemu hii inaongozwa na Sheria za Kanisa kuhusu Liturujia, ili waweze kuongozwa na Roho Mtakatifu katika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Lengo ni kuwapatia Makardinali fursa ya kuweza kusali na kutafakari bila kuwa na haraka, kwani mambo mazuri hayataki haraka ndivyo wanavyotujuza Waswahili. Ni kipindi ambacho Makardinali wanajiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza bila kushinikizwa na watu au sera za makundi ya kijamii. Papa anayechaguliwa kimsingi ni mtu ambaye anatarajiwa kuweza kukabiliana na changamoto za Kanisa kwa wakati wake, kama inavyojionesha pia katika kiapo na kura wanazopiga. Kura zinapigwa mara mbili: ya kwanza inapigwa asubuhi na kura ya pili inarudiwa jioni, ili kuwapatia Makardinali mwelekeo wa kuamua ni yupi kati ya wale ambao wamependekezwa anayeweza kwa nguvu ya Roho Mtakatifu kuliongoza Kanisa. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kunako mwaka 2007 aliamua kwamba, ili Kardinali aweze kuchaguliwa kuwa Papa lazima apate theluthi tatu ya kura zote halali na kwamba, “Conclave” inaweza kufanyika mapema kadiri ya maamuzi ya Makardinali kwa kusoma alama za nyakati na hivi ndivyo itakavyokuwa. Sheria na kanuni zinazoongoza uchaguzi wa Papa Mpya ni nyeti na adhabu yake ni kujitenga na Kanisa mara moja pasipo na huruma yaani kwa lugha ya sheria za Kanisa hali kama hii inajulikana kama “Latae Sententiae.”
Lengo ni kulinda uhuru wa Makardinali katika mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huu ni mwelekeo wa maisha ya kiroho unaooneshwa wakati wa Conclave. Hapa hakuna ushawishi kutoka nje, kama inavyojionesha kwa sasa, kila upande ukiwapigia “debe” Makardinali wanaodhani kwamba, wanaweza kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ikumbukwe kwamba, kwa Kardinali kuchaguliwa kuliongoza Kanisa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ni dhamana nyeti inayogusa utume wake. Huu si “ujiko” au fahari ya mtu. Hivi karibuni kumekuwepo na kampeni kubwa iliyofanywa na baadhi ya vyombo vya habari kwa kuwachafua watu pamoja na kuwawekea vizingiti kiasi kwamba, hawataweza kushiriki katika uchaguzi wa Papa Mpya. Hapa waamini wakumbuke kwamba, huu si uchaguzi wa kisiasa kama wengi walivyozoea. Kanisa lina imani na Roho Mtakatifu atakaye wawezesha Makardinali kufanya maamuzi ya busara pasipokuwa na shinikizo kutoka sehemu yoyote ile!