Tafuta

Mkutano wa 4 wa Makardinali. Mkutano wa 4 wa Makardinali.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mkutano wa makardinali:Dominika masifu ya jioni yatafanyika katika kaburi la Papa Francisko

Walishiriki makardinali 149 katika mkutano wa Ijumaa Aprili 25,ambapo wamezungumzia Kanisa na ulimwengu na hata mazishi ya Papa.Mshehereshaji wa Maadhimisho ya Liturujia za Kipapa alieleza kwamba,kadiri ya wosia wa Baba Mtakatifu,mazishi yatakuwa kama ya mchungaji,badala ya kuwa ya mfalme.Mwili hautaoneshwa kwenye catafalque.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Dominika alasiri, tarehe 27 Aprili 2025, Makardinali watakwenda katika Basilika ya Mtakatifu  Maria Mkuu jijini Roma kutembelea kaburi la Papa Francisko na kikanisa ambacho Picha yake mpendwa, ya Salus Populi Romani, inaonyeshwa humo. Pia watapitia Mlango Mtakatifu na kusali masifu ya jioni  pamoja. Hili ndilo lililoamuliwa katika mkutano mkuu wa nne wa makardinali ambao ulifanyika asubuhi ya Ijumaa tarehe 25 Aprili 2025 kuanzia saa 3.10 hadi saa 6.20 mchana masaa ya Ulaya, kwa mujibu wa ripoti kutoka kwa Dk. Matteo Bruni, Msemaji wa Vyombo vya habari Vatican.

Wakat wa ibada ya kuhamisha mwili

Katika mkutano huo kulikuwa na Makardinali 149 waliohudhuria katika Ukumbi wa Sinodi na kulikuwa na mada 33 zilizojadiliwa katika masuala mbalimbali yakiwemo mada za Kanisa na Ulimwengu. Kama katika vikao vingine, kutoka vifungu vya Katiba ya Kitume ya 'Universi Dominici Gregis', iliendelea na Makardinali waliofika leo pia walipata fursa ya kula kiapo. Mkutano wa 5 utafanyika Jumatatu asubuhi tarehe 28 Aprili  2025 saa 3.00 kamili  masaa ya Ulaya.

Mbinu na utaratibu wa mazishi

Mwishoni mwa mkutano huo wa makardinali, Mshehereshaji wa Maadhimisho ya Liturujia za Kipapa, Askofu Mkuu  Diego Ravelli alizungumza na kufafanua ibada ya mazishi. Kwa hiyo "yatakuwa kama mazishi ya mchungaji, badala ya kuwa kama mfalme,” alisema. Kiukweli, mwili wa Papa hautaoneshwa kwenye (katafalque) yaani kiunzi kinachotumika kuegemeza jeneza wakati wa maadhimisho ya mazishi. Dk. Matteo Bruni alikumbusha kwamba mabadiliko haya yalichaguliwa na kubuniwa na Papa Francisko mwenyewe na kuidhinishwa mnamo mwaka 2024, wakati  wa toleo jipya la “Ordo Exsequiarum Romani Pontificis” yaani “Kanuni za maishi ya Papa wa Roma” ilipochapishwa.

Kutoa heshima ya mwisho
Kutoa heshima ya mwisho   (Vatican Media)

Ofisi ya Vyombo vya Habari pia ilieleza kwamba Jumamosi Aprili 26, katika Misa ya mazishi, watu wenye mamlaka ya nchi watapangwa kulingana na itifaki, yaani, katika mstari wa mbele marais wa Argentina, nchi ya Papa na Italia watakuwapo. Kisha kutakuwa na Wafalme na marais wengine kwa mpangilio wa alfabeti ya Kifaransa. Orodha kamili ya wajumbe itatolewa leo; Kwa mujibu wa taarifa za jana Alhamisi 24 Aprili, takriban wajumbe 130 walithibitishwa, wakiwemo wakuu wa nchi takriban 50 na watawala wafalme 10. Kwa hiyo watakuwa wameongezeka.

Msafara wa kwenda Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu

Baada ya Misa, msafara wa mazishi hautapita kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro, bali utarudi kwenye Kanisa kuu. Kisha, kwa gari ambalo litakuwa wazi ili kuruhusu jeneza kuonekana, litatolewa katika mji wa Vatican kupitia Mlango wa Perugino, kuelekea kwenye Basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu. Safari hiyo inakadiriwa kuchukua kati ya dakika 30 na 40 na gari la kubeba mwili wa Papa litaenda kwa kasi ya takriban 10km kwa saa. Picha za msafara huo zitaoneshwa moja kwa moja kwenye chaneli za Vyombo vya Habari vya Vatican na matangazo yataisha baada ya kuwasili kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu. Wakati huo huo Saa 3.00 kamili usiku, Kardinali Rolandas Makrickas ataongoza Rozari Takatifu kwa ajili ya kumuombea Hayati Papa Francisko itakayofanyika nje ya Basilika.

Waamini 150elfu wametoa heshima kwa Papa na waandishi wa habari 2700 

Kufika jioni ya leo  Kanisa kuu la Mtakatifu Petro litafungwa saa 1:00 jioni masaa ya Ulaya, lakini foleni hiyo utaisha saa 12:00, ili kuwapa nafasi waamini kuaga Papa, kabla ya ibada ya kufunga jeneza, ambayo itakuwa ni kitendo cha faragha. Tangu Jumatano 23 Aprili iliyopita hadi saa 6:00 kamili mchana wa leo 25 Aprili, takriban watu 150,000 wamemiminika kwenye Kanisa Kuu la Vatican kutoa heshima kwa Baba Mtakatifu. Ofisi ya Vyombo vya Habari pia inaripoti kwamba angalau waandishi wa habari 2,700 kutoka ulimwenguni kote wameidhinishwa kwa matukio ya siku hizi.

25 Aprili 2025, 18:16