Tafuta

Papa Pio XII kunako Mei Mosi, 1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo, mfano na mwombezi wa wafanyakazi wote duniani. Papa Pio XII kunako Mei Mosi, 1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo, mfano na mwombezi wa wafanyakazi wote duniani.  (AFP or licensors)

Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi: Mei Mosi Sikukuu ya Wafanyakazi 2025

Mama Kanisa katika huruma na upendo wake usiokuwa na kifani, ili apate kuwalinda na kuwatuliza wafanyakazi, sehemu mbalimbali za dunia, Papa Pio XII kunako Mei Mosi, 1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo, mfano na mwombezi wa wafanyakazi wote duniani, atakayewasaidia kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao, ili kujenga na kudumisha utu, heshima, haki msingi, mshikamano na udugu wa kibinadamu: Kazi kama utimilifu wa utu na heshima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani. Lengo ni kuhamasisha utoaji wa haki msingi kwa wafanyakazi, kuboresha masharti ya kazi ili kuongeza tija na ufanisi zaidi sanjari na kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wafanyakazi wengi. Katika maadhimisho haya, Jumuiya ya Kimataifa inapenda kutambua na kuenzi mchango wa wafanyakazi katika sekta mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Mei Mosi, ni siku maalum ya kuonesha umoja na mshikamano kati ya wafanyakazi, sanjari na kuhimiza usawa na haki katika maeneo ya kazi, sehemu mbalimbali za dunia. Mei Mosi ni kumbukumbu ya mauaji ya halaiki yaliyotokea kunako mwaka 1886 katika viwanja vya Haymarket Chicago, nchini Marekani. Polisi walikuwa wakitawanya mkusanyiko wa wafanyakazi wakati wa mgomo wa kupinga masaa nane ya kazi ambapo mtu asiyejulikana aliwarushia askari bomu. Polisi waliwalirushia risasi wafanyakazi hao na hivyo kupelekea vifo vya wafanyakazi wanne. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo muhimu sana katika sera na mikakati ya shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Binadamu wanapaswa kuangaliana na kuchukuliana kama ndugu wamoja na kwamba, kazi nzima ya uumbaji ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na inashangaza sana machoni pa binadamu! Kazi inamtambulisha mwanadamu na kumwezesha kutekeleza karama na mapaji mbalimbali aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yake. Kwa njia ya kazi, mwanadamu anashiriki pia katika mpango wa kazi ya uumbaji iliyoanzishwa na Mwenyezi Mungu na hivyo kushiriki pia katika mchakato wa mshikamano na jirani zake. Licha ya shida na magumu yanayojitokeza katika kazi, lakini inamwezesha mtu kukua na kukomaa, pamoja na kutekeleza ndoto za maisha yake.

Usalama kazini ni jambo la muhimu ili kuongeza tija na ufanisi
Usalama kazini ni jambo la muhimu ili kuongeza tija na ufanisi

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakazia kuhusu haki msingi za wafanyakazi, vinginevyo watageuka na kuwa ni watumwa wa kazi, Mama Kanisa katika huruma na upendo wake usiokuwa na kifani, ili apate kuwalinda na kuwatuliza wafanyakazi, sehemu mbalimbali za dunia, Papa Pio XII kunako Mei Mosi, 1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo, mfano na mwombezi wa wafanyakazi wote duniani, atakayewasaidia kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao, ili kujenga na kudumisha utu, heshima, haki msingi, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kwa vile Sikukuu hii iligubikwa sana na kilio cha wafanyakazi, machafuko, kinzani na misigano, hasa kwenye Karne ya Kumi na tisa, Mama Kanisa akataka Mtakatifu Yosefu kuwa ni kielelezo makini cha mapambano ya kudai haki msingi za wafanyakazi, utu na heshima yao pamoja na kutoa hadhi kwa kazi kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa kazi ya uumbaji na ukombozi ambayo hata Kristo Yesu mwenyewe aliishiriki kiasi hata cha watu kumsema: “Huyu si yule seremala…” Mk. 6:3. Mkazo kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanafanya kazi kwa: bidii, juhudi na maarifa, ili kuweza kujipatia: mali na mapato halali; kwa kutambua na kuheshimu kazi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatumia rasilimali za dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao.

Utu, heshima na haki za wafanyakazi ziheshimiwe.
Utu, heshima na haki za wafanyakazi ziheshimiwe.   (ANSA)

Hayati Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Mei Mosi, 2024 aliwakumbusha waamini na mahujaji waliohudhuria Katekesi yake kwamba, Mei Mosi, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi na mwanzo wa mwezi Mei, uliotengwa kwa ajili ya heshima na ibada kwa Bikira Maria. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuiga mfano bora wa Familia Takatifu ya Nazareti ya Mtoto Yesu, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, ili familia zao, Kanisa dogo la nyumbani, liweze kuwa ni Jumuiya ya maisha, kazi na upendo. Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi, awasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa kuwaelekeza watu kwa Kristo Yesu. Awalinde na kuwasaidia wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, awaombee wale wote ambao wamepoteza fursa za ajira na kazi au ambao bado wanachakarika usiku na mchana kutafuta fursa za kazi! Kanisa ni Mama na Mwalimu, daima anapenda kushikamana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utu, heshima na haki msingi za binadamu hazina budi kupewa kipaumbele cha kwanza. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, kazi iliyotekelezwa na Mtakatifu Yosefu, ni kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu aliyemuumba mwanadamu, anathamini sana kazi ya uumbaji aliyoitekeleza kwa muda wa siku sita na siku ya saba akapumzika. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mtakatifu Yosefu, Msimamizi wa wafanyakazi, aendelee kuwakumbuka na kuwaombea watu wote, ili asiwepo kijana, familia au mtu awaye yote asiyekuwa na fursa ya ajira. Hii iwe ni dhamana inayowawajibisha watu wote.

Kuna watu wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi
Kuna watu wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi   (AFP or licensors)

Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Kazi Duniani, ILO, mwaka 2019, Hayati Baba Mtakatifu Francisko alikazia mambo makuu yafuatayo: Umuhimu wa kazi kama utimilifu wa mtu binafsi, kijamii na kiikolojia; leo hii kuna haja ya kutengeneza na kulinda fursa za ajira duniani kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi mintarafu mapokeo, rasilimali muda na teknolojia. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anatambua na kuthamini umuhimu wa kazi kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa amani duniani, haki jamii pamoja na kuendeleza maboresho ya kazi. Licha ya juhudi zote hizi, bado kuna ukosefu mkubwa wa fursa za ajira duniani; kuna watu wanaonyonywa na kudhalilishwa utu na heshima yao katika biashara ya binadamu na utumwa mamboleo bila kusahau kazi za shuruti na ujira “kiduchu”. Kuna watu wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi bila kusahau uchafuzi mkubwa wa mazingira, hali ambayo pengine inachangiwa na mbinu za kiteknolojia na matumizi yake!

Mtakatifu Yosefu Mei Mosi 1955 Msimamizi wa wafanyakzi duniani
Mtakatifu Yosefu Mei Mosi 1955 Msimamizi wa wafanyakzi duniani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu anafafanua kuhusu dhana ya kazi kama utimilifu wa mtu binafsi, kijamii na kiikolojia, kwa kusema kwamba, kazi ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, kazi ni wito wa mwanadamu. Hapa ni mahali pa kubadilishana mawazo, mang’amuzi na uzoefu wa maisha; ni mahali pa kujenga mahusiano kwa kukutana na watu wengine, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na ujenzi wa utamaduni wa upendo. Wito wa kazi una uhusiano wa pekee na mazingira nyumba ya wote, ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu kuyalinda, kuyatunza na kuyaendeleza kama sehemu ya ikolojia ya maisha ya mtu binafsi, jamii na dunia katika ujumla wake. Kazi kamwe haiwezi kuhesababiwa kuwa ni sehemu ya mnyororo wa uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma kwa ajili ya kutengeneza mtaji. Kanuni maadili ni muhimu sana katika kulinda na kuzalisha fursa za ajira kama sehemu ya utimilifu wa maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutengeneza na kulinda fursa za ajira ajira duniani na kwamba, fursa za ajira zinapaswa kuangaliwa kwa mwanga wa masuala ya kijamii-kisiasa na kiuchumi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa linapenda pia kuchangia katika mchakato huu kupitia Shirika la Kazi Duniani. Mfumo wa uchumi unapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, kwa kulinda na kudumisha mazingira nyumba ya wote, kwa ajili ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.

Wafanyakazi wakiandamana kudai haki zao
Wafanyakazi wakiandamana kudai haki zao   (ANSA)

Binadamu anapaswa kuwa ni kiini na hatima ya sera na mikakati ya maendeleo fungamani kwa kukazia: umuhimu wa ardhi, makazi na ajira. Ardhi ni amana na utajiri wa binadamu wote na matunda yake ni kwa ajili ya wote. Kila mtu anayo haki ya kutumia ardhi kwa ajili ya mafao yake. Hii ni kanuni maadili inayolinda utaratibu wa maisha. Kuna uhusiano na mwingiliano mkubwa kati ya kazi na mazingira na kwamba, kuna baadhi ya shughuli za binadamu zinazosababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira, kwa kuzalisha hewa ya ukaa. Jumuiya ya Kimataifa inapoweka sera na mikakati ya kulinda fursa za ajira, haina budi kuhakikisha kwamba inazingatia mwingiliano kati ya ardhi, makazi na ajira. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, mapokeo “tradion” kutoka katika mzizi neno wa lugha ya Kilatini “tradere” yaani kurithisha, si tu teknolojia, bali pia uzoefu, dira na matumaini, kwa ajili ya ustawi wa binadamu na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote! Rasilimali muda imekuwa ni changamoto kubwa kwani muda umekuwa ni kikwazo cha maendeleo na maboresho ya maisha ya watu kutokana na kasi kubwa na hivyo watu kushindwa kutambua kwamba, rasimali muda ni zawadi kutoka kwa Mungu inayopaswa kupokelewa, kudumishwa na kuthaminiwa kama sehemu ya mchakato wa maendeleo ya mwanadamu. Watu wanahitaji rasilimali muda kwa ajili ya kazi, kupumzika na kutafakari uzuri wa kazi ya uumbaji.

Sikukuu ya wafanyakazi duniani
Sikukuu ya wafanyakazi duniani   (ANSA)

Rasilimali muda ni muhimu katika kupanga na kutekeleza majukumu mbalimbali ya maisha. Jamii inahitaji kusimama na kutulia, ili kugundua thamani ya muda badala ya kukimbizana na wakati! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, teknolojia ni muhimu sana na kamwe isiwajengee watu kiburi cha kuwa na nguvu, kutaka kuwatala na kuwamiliki wengine au kuwachezea kama wanavyopenda. Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi katika mfumo wa kidigitali, matumizi ya roboti pamoja na matumizi ya teknolojia akili unde, AI, yote haya yanaendelea kuleta mageuzi makubwa katika ulimwengu wa kazi na mahali wanapoishi watu! Mabadiliko haya ni makubwa, kumbe, yanapaswa kuongozwa na kusimamiwa na sheria mpya, kanuni maadili na utu wema ili kudhibiti kazi za suluba kwa watoto wadogo au ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana wa kizazi kipya! Hayati Baba Mtakatifu alilipongeza Shirika la Kazi Duniani, ILO kwa kuendelea kupambana na kazi za suluba kwa watoto wadogo, kiasi cha kuwapoka ndoto na matumaini yao ya kuweza kuchangia ustawi na maendeleo ya jamii kwa siku za usoni. Ukosefu wa fursa za ajira na usalama kazini ni matokeo ya mfumo wa uchumi kandamizi unaotaka kunyonya nguvu kazi na mazingira, kwa kumweka mwanadamu pembezoni mwa vipaumbele vya kiuchumi. Hizi ni dalili za ukosefu wa sera na mikakati makini inayopaswa kutumika kwa ajili ya kurekebisha mwelekeo huu, ili haki iweze kutendeka. Shirika la Kazi Duniani, ILO kwa kushirikiana na Kanisa linaweza kusaidia kuwaundia watu hisia za utunzaji bora wa mazingira, sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kwa kuunganisha mapokeo, rasilimali muda na teknolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafo ya wengi. Mwishoni, Baba Mtakatifu analitaka Shirika la Kazi Duniani, kuendelea kushughulikia changamoto changamani za kazi kwa ari na moyo mkuu!

Mei Mosi 2025

 

 

30 Aprili 2025, 16:07