Papa Francisko: Tafakari Njia ya Msalaba Kuzunguka Magofu ya Colloseo 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jina Takatifu la Yesu linafafanua ndani mwake: Fumbo la Umwilisho linalopata hatima yake katika Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko uletayo uzima wa milele. Hili ni jina linalofumbata tunu msingi za Kristo Yesu yaani: Ufukara, maisha, utume na kazi alizotenda Kristo Yesu kwa ajili ya kufunua na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake. Maandiko Matakatifu yanakaza kusema “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu." Mt 1:21. Kumbe, hili ni jina kadiri ya Maandiko Matakatifu linalofafanua utume wa Yesu, yaani “Mungu anaokoa.” Vituo vya Njia ya Msalaba ni sala ya watu wanaotembea, huku wakikabiliana na changamoto mbalimbali na hivyo kuwawezesha kuvuka kutoka katika uchovu na hali ya kutojali na hivyo kuelekea kwenye furaha ya kweli. Kumfuasa Kristo katika Njia ya Msalaba kuna gharama yake na huo ni mwanzo wa maisha mapya, toba na wongofu wa ndani; Upatanisho na uchaji wa Mungu, tayari kusikia tena mwaliko kutoka kwa Kristo Yesu, “Njoo na matumaini katika mtazamo wa upendo.” Magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma nchini Italia ni uwanja maarufu sana uliokuwa unatumika kwa ajili ya kuwashindanishia binadamu na wanyama, kielelezo cha ukatili na mateso katika maisha ya mwanadamu. Mama Kanisa katika Ibada ya Ijumaa kuu kila mwaka anayatumia Magofu ya Colosseo kwa ajili ya kutafakari Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Yesu anawaambia wafuasi wake kwamba, mtu anayetaka kumwona, yaani kumwamini kwa dhati kabisa hana budi kumwangalia ndani kabisa ya Fumbo la Msalaba, ambalo linafunua utukufu na ukuu wake kama Mwana wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuyainua macho yao juu ya Msalaba wa Kristo ili kumtafakari na hatimaye, kumfahamu. Kwa bahati mbaya, Msalaba umekuwa ukitumiwa na baadhi ya watu kama “mapambo tu”, lakini kwa waamini, Msalaba ni ufunuo wa Fumbo la Mateso na Kifo cha Mwana wa Mungu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Mungu, chemchemi ya msamaha, upatanisho, maisha mapya na wokovu kwa binadamu wa nyakati zote!
Kwa njia ya Madonda yake Matakatifu, watu wote wamepata kuponywa! Katika hali na mazingira kama haya, wajitahidi kuona na kuguswa na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, pale juu Msalabani, Kristo Yesu, ametundika mateso na mahangaiko ya binadamu wote. Akiwa ametundikwa Msalabani, watu wengi walimdhihaki, wakamtukana na kumdhalilisha; wakamchoma mkuki ubavuni, na hatimaye, akafa kifo cha aibu. Kristo Yesu katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi. Katika shida na mahangaiko ya binadamu, Kristo Yesu, aliweza kuhuzunika, akatoa machozi, akawa faraja na chombo cha baraka kwa wale waliokuwa wanamzunguka. Katika shida na magumu ya maisha, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, wawe wepesi kumkimbilia na kumwangalia Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani, ili kujiaminisha na kujikabidhi katika ulinzi na tunza yake. Yesu ni jibu makini katika mateso na mahangaiko ya binadamu. Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo Ijumaa kuu tarehe 18 Aprili 2025 imeandaliwa na Baba Mtakatifu Francisko na inaongozwa na Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma. Njia hii ya Msalaba inamwonesha Kristo Yesu akitekeleza dhamana na wajibu wake wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Huu ni Msalaba unaovunjilia mbali kuta za utengano; unaopania kufuta deni kubwa linalozielemea Nchi changa duniani kiasi cha kufifisha harakati za ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni Msalaba unaopania kufuta adhabu ya kifo, inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; ili hatimaye, kuanzisha mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa kweli. Kristo Yesu ndiye Jubilei ya kweli, anayeonesha ujirani mwema hata kwa watesi wake, kwa hakika Kristo Yesu anapania kuwakomboa watu wote kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Katika Njia hii ya Msalaba, Kristo Yesu anaonesha unyenyekevu, uaminifu na utii kwa Baba yake wa mbinguni, muhtasari wa Heri za Mlimani, kiini cha mafundisho yake makuu kwa wafuasi wake. Hiki ni kielelezo cha Uchumi wa Kimungu, chanzo cha uhai na maisha mapya. Huu ni uchumi unaowajibisha na hivyo kuwaondoa waamini kutoka katika uchoyo, ubinafsi na hali ya kutojali wala kuguswa na mateso, mahangaiko na changamoto zinazowakumba wengine. Baba Mtakatifu katika Sala ya Utangulizi wa kila Kituo cha Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari, anawaangalia wakimbizi na wahamiaji, wanaotafuta: Hifadhi, usalama, ustawi na maisha bora zaidi. Kumbe, Sala ya Njia ya Msalaba ni sala ya wakimbizi na wahamiaji. Hii ni njia ambayo ina gharama zake na ikiwa kama watapokelewa kama zawadi, kwa hakika anasema Baba Mtakatifu Francisko huo unakuwa ni mwanzo mpya unaochanua na hivyo kuleta maisha mapya; mwanzo wa msamaha na upatanisho wa kweli; toba na wongofu wa ndani unaoweza kubadilisha hata moyo wa jiwe, kuwa ni moyo wa nyama. Pilato anamhukumu Kristo Yesu ingawa haoni kosa lake, anawaogopa Wayahudi, anapenda kupalilia urafiki na Kaisari. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hivi ndivyo ilivyo katika Ulimwengu mamboleo, kuna watu wanashitakiwa na kuhukumiwa bila kosa, wanabeba adhabu zao kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba, akaonesha kimya kikuu mbele ya watesi wake. Akaelemewa na Msalaba kiasi cha kuanguka mara tatu. Ukimya wa Kristo Yesu ni kielelezo cha malumbano ya kidini na kisheria; hali ambayo haiangalii na kugusa hatima ya watu wengine na hivyo watu wengi wanajikuta wakiwa wamevaa dhamana ya: Herode, Makuhani, Pilato na Umati mkubwa wa watu wanaotaka Kristo Yesu, ahukumiwe adhabu ya kifo, ili atoweke katika uso wa dunia, lakini hata katika hili, Kristo Yesu katika hali ya kimya kikuu, anaendelea kuonesha upendo mkubwa.
Uhuru wa kweli unakita mizizi yake katika kufikiri, kuamua na kutenda, chimbuko la imani, matumaini na uhuru wa ndani. Mama Kanisa anapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa: Amani, uhuru wa kidini, utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani ya binadamu, kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hizi ni haki za wote zisizoweza kukiukwa wala kutenguliwa. Ni za binadamu wote bila kujali: wakati, mahali au mhusika. Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Haki ya kwanza kabisa ni uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale anapofariki dunia kadiri ya mpango wa Mungu. Mkazo umewekwa katika haki ya uhuru wa kidini inayofafanuliwa katika uhuru wa kuabudu. Hiki ni kiini cha haki msingi kinachofumbata haki nyingine zote. Kuheshimu na kuthamini haki hii ni alama ya maendeleo halisi ya binadamu katika medani mbalimbali za maisha. Haki inakwenda sanjari na wajibu! Mama Kanisa anakazia kwa namna ya pekee kabisa, umuhimu wa kuheshimu haki msingi za binadamu, kichocheo muhimu sana cha amani na utulivu miongoni mwa binadamu. Kanisa linapenda kusimama kidete: kulinda na kudumisha haki na amani sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mwanga na chachu ya tunu msingi za Kiinjili! Kusamehe na kusahau ni chemchemi ya utakatifu wa maisha, kama anavyoonesha Kristo Yesu kwa kuwaombea msamaha watesi wake kwani walikuwa hawajui watendalo, mwanzo wa Njia ya Msalaba inayowaongoza waamini kwenda kwa Mungu Baba Mwenyezi.
Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake ya Njia ya Msalaba anasema Kristo Yesu alianguka mara tatu, akasimama na kuendelea na safari yake kuelekea mlimani Kalvari, kumbe, kuna umuhimu kwa waamini kujenga utamaduni wa kusoma alama za nyakati; wajifunze kusimama tena baada ya kuanguka; Kusamehe na kusahau kama alivyotend Kristo mwenyewe na hivyo kujikita katika uchumi unaoheshimu utu, haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu asiye na dhambi, amewapenda wote na kuwakumbatia; amejitahidi kuwainua kwa misingi ya ujasiri na ukarimu. “Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika Msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.” Lk 23:26. Msalaba huu ulikuwa ni mzito, changamoto na mwaliko kwa waamini katika Njia ya Msalaba kumtafakari Simoni Mkirene, kwa kuuangalia moyo wake na hatua zake pamoja na Kristo Yesu. Katika Njia ya Msalaba kuna wahusika wengi wanaoonesha hisia zao na uzoefu, lakini Simoni Mkirene, alijifunza kujivika nira na kubeba mzigo wa Yesu ambao ni laini, mwaliko kwa waamini kujifunza kushiriki katika maisha na utume wa Kristo Yesu; kwa kumpatia kipaumbele cha kwanza Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Wanawake wa Yerusalemu wanatajwa pia katika Njia ya Msalaba na kwamba, Mama na ndugu zake Kristo Yesu ni wale wanaosikiliza na kutenda kadiri ya mapenzi ya Kristo Yesu. Hawa ndio akina Mariam na Veronika aliyethubutu kuupangusa uso wa Yesu, changamoto na mwaliko wa kujenga utamaduni wa upendo kwani upendo una nguvu zaidi ya kifo na kwamba, kwa njia ya upendo, watu huweza kubadilika na hivyo kuonja wema na huruma ya Mungu na hivyo kuchochea ujenzi wa mahusiano na mafungamano bora zaidi.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, katika ulimwengu ambamo watu wengi wamepondeka na kuvunjika moyo, machozi ya dhati ni muhimu. Kristo Yesu alihitimisha safari yake ya Njia ya Msalaba, kwa kushushwa chini na hatimaye, Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu, (lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake. Yn 19: 35. Yusufu wa Arimathaya alikuwa ni mtu wa matumaini na mtetezi wa haki, mwaliko kwa waamini kuwajibika barabara: kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha tafakari yake ya Njia ya Msalaba kwa Mwaka 2025 kwa kuwaomba waamini kujifunza ukimya, Jumamosi kuu, baada ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani na hatimaye kuzikwa kaburini na kudhani kwamba, huo ndio mwisho wa safari ya Njia ya Msalaba, lakini ufufuko wake ni kielelezo cha uumbaji mpya na chanzo cha amani kati ya Mataifa.