Tafuta

Papa:Usiegeshe moyo katika udanganyifu wa dunia,tukimbie kuelekea Kristo!

Katika misa ya Pasaka Aprili 20,2025 katika uwanja wa Mtakatifu Petro iliyoongozwa na Kardinali Comastri kwa niaba ya Papa katika mahubiri ni mwaliko kwa waamini kuwa na matumaini kwamba tunaweza kuishi maisha haya dhaifu,tete na yenye majeraha tukishikamana na Kristo,kwa sababu ameshinda kifo,anashinda giza letu na atashinda giza la dunia.Jubilei inatualika kujipyaisha ndani mwetu zawadi ya tumaini ili kuingiza ndani mwake mateso yetu na kutotulia kwetu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika Sherehe ya Pasaka, Siku ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, Dominika tarehe 20 Aprili 2025, misa ya asubuhi iliyoadhimishwa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican saa 4.30  masaa ya Ulaya ikiwa ni saa 5.30 masaa ya Afrika Mashariki, iliongozwa na Kardinali Angelo Comastri, Askofu Mkuu Mstaafu  na makamu wa  Baba Mtakatifu katika mji wa Vatican na Askofu Mkuu mstaafu wa Basilika ya  Mtakatifu Petro ambaye alichaguliwa na Papa kumwakilisha katika siku kuu hii wakati yeye anaendelea kupata nafuu baada ya kulazwa hospitalini. Katika mahubiri ya Baba Mtakatifu yanaanza  na nukuu ya kifungu cha Injili isemayo: Maria na Mgdalena kwa kuona jiwe lililokuwa  limeviringishwa, walianza kukimbia kwenda kuwaeleza Petro na Yohane. Hata mitume wawili baada ya kupata habari za kushangaza, Injili inasema walitoka na kukimbia pamoja wote wawili (Yh 20,4).

Misa ya subuhi ya Pasaka 2025
Misa ya subuhi ya Pasaka 2025   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Wahusika wa simulizi ya Pasaka wanakimbia wote! Kukimbia huku, kunajieleza kwa upande mmoja, wasiwasi waliokuwa nao wa kuondolewa kwa mwili wa Bwana: lakini upande mwingine, kimbia ya Magdalena, Petro na Yohane inaeleza shauku, msukumo wa moyo, tabia ya ndani kwa yule anajiweka katika utafutaji wa Yesu. Yeye kiukweli ni mfufuka kutoka katika wafu na kwa hiyo hayupo tena kaburini. Lazima kumtafuta mahali pengine. Hili ni tangazo la Pasaka: lazima kumtafuta mahali pengine. Kristo amefufuka, anaishi! Yeye hakubaki mfungwa wa kifo, hakufungwa tena mashuka ya maziko, na kwa hiyo huwezi kumfunga katika historia nzuri ya kusimulia, huwezi kumfanya yeye shujaa wa wakati uliopita au kumfikiria kama sanamu iliyowekwa vizuri katika ukumbi wa makumbusho! Kinyume chake, lazima kumtafuta na hivyo hatuwezi kubaki tumesimama. Lazima tujiweke  safarini, tutoke kwenda kumtafuta: kutamfuta katika maisha, kumtafuta katika nyuso za ndugu, kumtafuta katika maisha ya kila siku, kutamfuta kila mahali, lakini siyo kabuni. Kumtafuta daima.

Misa ya Asubuhi ya Pasaka
Misa ya Asubuhi ya Pasaka   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kwa sababu ikiwa amefufuka kutoka katika kifo, kwa hiyo Yeye yupo kila mahali, anakaa katikati yetu, anajificha, na anajionesha hata leo hii kwa dada na kaka zetu tunaokutana nao katika safari yetu, katika hali zetu zisizojulikana zaidi na katika yasiyotarajiwa ya maisha yetu. Yeye anaishi na anabaki daima na sisi, kwa kulia machozi na yule anayeteseka na kwa kuzindisha uzuri wa maisha katika ishara ndogo ndogo za upendo wa kila mmoja wetu. Kwa njia hiyo imani ya Pasaka, ambayo inatufungulia mkutano na Bwana Mfufuka, na tunajitayarisha kuipokea katika maisha,  si kitu kingine ambacho kimeandaliwa na kutulia, na suluhisho la amani katika uhakikisho fulani wa kidini. Kinyume chake, Pasaka inatukabidhi mwendo, inatusukuma kukimbia kama Maria Magdalena na kama mitume; inatualika kuwa na uwezo wa “mtazamo wa kuona mbali,” ili kumtambua Yesu, aliye hai, kama Mungu ambaye anajionesha na hata leo hii yupo, anazungumza nasi, anatutangulia na kutushangaza.

Kama Maria Magdalena, kila siku tunaweza kufanya uzoefu wa kumpoteza Bwana, lakini kila siku pia sisi tunaweza kukimbia kumtafuta bado, kwa kujua kwa hakika kuwa Yeye anapatikana na anatuangazia na mwanga wake wa ufufuko. Kwa hiyo Papa alisisitiza kuwa: “Kaka na dada, haya ni matumaini makubwa zaidi ya maisha yetu: tunaweza kuishi maisha haya maskini, dhaifu na majeraha kwa kung’ang’ania kwa Kristo, kwa sababu Yeye alishinda kifo, anashinda giza zetu na atashinda giza la Ulimwengu ili kutufanya tuishi naye katika furaha milele. Katika kuelekea hatima hiyo, kama anavyosema Mtume Paulo, hata sisi tunakimbia kwa kusahau kile kilichopo mabegani mwetu na kuishi kwa kuelekea kile ambacho tunatazamia (Fil 3,12-14). Tuharakishe kwa hiyo kwenda kukutana na Kristo, kwa hatua za haraka kama Magdalena, Petro na Yohane.

Misa ya asubuhi ya Pasaka 2025
Misa ya asubuhi ya Pasaka 2025   (Vatican Media)

Jubilei inatualika kujipyaisha ndani mwetu zawadi hii ya  tumaini , kuingiza ndani mwake mateso yetu na mateso ya kutotulia kwetu, ili kuambukiza wale ambao tunakutana nao katika safari, kukabidhi tumaini hili la wakati ujao, la maisha yetu na hatima ya ubinadamu. Na kwa hivyo hatuwezi kuegesha moyo kwenye udanganyifu wa ulimwengu huu au kuufungia katika huzuni; tunapaswa kukimbia, tukiwa tumejaa furaha. Tukimbie kukutana na Yesu ili tugundue neema na thamani isiyo na kifani ya  kuwa marafiki zake. Hebu tuache Neno liwe maisha na ukweli unaoangaza safari yetu.  Kama alivyotaka  kusema Mtaalimungu Mkuu, Henri de Lubac kuwa, inatosha kuelewa hili kwamba: “Ukristo ni Kristo. Hakuna, kweli hakika ya chochote zaidi ya hicho. Katika Kristo, sisi ni yote,” (Les responsabilités doctrinales des catholiques dans le monde d’aujourd’hui, - Wajibu wa mafundisho ya Wakatoliki katika ulimwengu wa leo, Paris 2010, 276).

Misa ya asubuhi ya Pasaka 2025
Misa ya asubuhi ya Pasaka 2025   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Na hii ya “Yote,” ambayo ni Kristo Mfufuka, inafungua maisha yetu katika matumaini. Yeye yuko hai, Yeye  leo hii bado anataka kupyaisha maisha yetu. Kwake yeye mshindi wa dhambi na wa kifo tunataka kusema:  Ee Bwana katika sherehe hii, sisi tunakuomba zawadi hii ya kuweza kuwa  wapya wa kuishi mapya milele.  Ee Mungu, futa  kwetu tabia ya mavumbi ya kusikitisha, ya uchovu na kukata tamaa; utupatie furaha ya kuamka, kila asubuhi na mtazamo wa  mshangao ili kuona rangi za kushangaza za asubuhi, za kipekee na tofauti kwa kila mmoja(…) Yote ni mapya, Ee Bwana na hakuna kilichorudia, na hakuna kipya(A. Zarri,Quasi una preghiera). Kwa kuhitimisha, Baba Mtakatifu anatoa mwaliko kuwa: Kaka na dada, katika mshangao wa imani ya Pasaka, kwa kuubeba katika moyo wa kila tarajio la amani na la ukombozi, tunaweza kusema: “Pamoja nawe Ee Bwana, kila kitu ni kipya, yote huanza.”

Misa ya Pasaka asubuhi
Misa ya Pasaka asubuhi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kardinali Angelo Comastri, mwishoni mwa mahubiri, alitaka kumshukuru Baba Mtakatifu kwa "mwaliko huu mkubwa wa kuamsha imani yetu.” Misa imeudhuliwa, karibu waaminifu elfu 35 wamekusanyika katika katika Uwanja wa Mtakatifu. Miongoni mwao walikuwa Waziri Mkuu wa Croatia Andrej Plenković na ujumbe kutoka Uholanzi. Kama kila mwaka, uwanja wa mbele ya Basilika ya Vatican ulipambwa kwa maua na mimea ya kila aina na rangi kwa Juma Takatifu. na mwaka huu Wakristo wa Mashariki na Magharibi wanasherehekea Pasaka pamoja katika siku hii ambapo Injili ilisomwa kwa Kigiriki na Kilatini. Nyimbo za Pasaka kutoka liturujia ya Byzantine pia ziliimbwa.

MISA ASUBUHI YA PASAKA
20 Aprili 2025, 11:57