Ujumbe wa Hayati Papa Francisko Kwa Vijana wa Kizazi Kipya: Jengeni Utamaduni wa Kusikiliza
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Parokia ya Mtakatifu Magdalena wa Canossa, Dominika tarehe 12 Machi 2017 alipata bahati ya kukutana na kuzungumza na watoto, wazazi na walezi wa watoto waliobatizwa katika kipindi cha mwaka 2016, wazee pamoja na wagonjwa. Akizungumza na watoto wadogo, Baba Mtakatifu aliweza kuwajibu maswali yao na kuwaambia watoto hawa kwamba, Yesu anapenda kuwa karibu sana na waja wake wanapomwendea kwa moyo mnyofu, toba na wongofu wa ndani! Yesu daima yuko tayari kukutana na waja wake ili kuwaonjesha huruma, upendo na msamaha katika maisha yao. Yesu daima yuko mioyoni mwao wakati wote wa maisha yao! Katika shida na magumu ya maisha, anawafariji. Baba Mtakatifu aliwapongeza Makatekista wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa; wako mstari wa mbele katika kufundisha Katekesi pamoja na kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika Parokia na Majimbo yao. Makatekista wanayo dhamana ya kufundisha: Imani ya Kanisa, Sakramenti, Amri za Mungu na Sala; hii ni dhamana nyeti sana.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya kijamii inayowawezesha watu wengi kuwasiliana! Lakini kwa bahati mbaya, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kimekuwa ni chanzo kikuu cha kusambaratika kwa mawasiliano katika familia na jamii katika ujumla wake. Badala ya kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi matokeo yake, hakuna tena utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana, watu wamezama sana katika matumizi ya teknolojia ya mawasiliano kiasi hata cha kushindwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wengine. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana katika ukweli na uwazi; kwa kuhudumiana katika huruma na upendo. Majadiliano ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa daraja la watu kukutana.
Ni katika muktadha wa kuwataka vijana kujifunza utamaduni wa kusikiliza ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa amani duniani, tarehe 8 Januari 2025 Baba Mtakatifu alirekodi ujumbe kwenye simu ya Luca Drusian aliyekuwepo kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha, mjini Vatican kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya. Hayati Baba Mtakatifu aliwaambia vijana kwamba, “kati ya mambo msingi katika maisha ni watu kujifunza utamaduni wa kusikiliza, kwa kumwachia nafasi jirani yako azungumze kabla ya kumkatisha, lengo ni kufahamu kikamilifu ujumbe anaotaka kukupatia.” Luca Drusian anajihusisha na ujenzi wa maabara ya utamaduni wa kusikiliza, mradi unaowahusisha vijana wa kizazi kipya na wazee, mintarafu tema mbalimbali za maisha, lengo likiwa ni kujenga utamaduni utakaowasaidia kutambua uzuri wa kusikilizwa, kusikiliza na hatimaye kusikia. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, leo hii watu wengi hawana utamaduni wa kusikiliza, kiasi kwamba, wanapenda kuingilia na kuwakatiza watu wengine wasiendelee kuzungumza, jambo hili ni hatari kwa muktadha wa ujenzi wa utamaduni wa kisikiliza. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, anawataka vijana wa kizazi kipya wajeneg utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kwamba, mababu na bibi zetu wametufundisha mengi. Haya ni maneno kuntu!