Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wa Pasaka Urbi et Orbi:2025:kupinga silaha na vita!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kama upepo mwanana sauti ya Papa Francisko ilienea katika jiji lote na dunia nzima. Ilikuwa yapasa taa 6.02 mchana ambapo mapazia mazito katikati ya Basilika ya Mtakatifu Petro eneo la kutoa Baraka, yalifunguliwa na kumruhusu Papa kuingia katika sehemu ambayo ni moyo wa Basilika ya Vatican. Baada ya majuma ya dhana na utabiri, kwa hiyo Baba Mtakatifu hatimaye alikuwa kwenye moja ya hafla muhimu zaidi katika maisha ya Kanisa, yaani katika kutoa baraka ya Pasaka Urbi et Orbi, yaani kwa Roma na ulimwengu, ambayo ni yeye anayepaswa kuitoa mwenyewe. Kuwasili kwa Papa kuliambatana na shangwe iliyoonekana na kusikika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na ambapo Mungu bariki aliwezesha jua, hata kama sio sana, lakini hapakuwa na mvua kama siku chache zilizopitia. Takriban waamini elfu 35 walikusanyika katika uwanja huo na ambapo muda mfupi walikuwa wameshiriki Misa ya Pasaka iliyoongozwa, kwa niaba ya Papa na Kardinali Angelo Comastri. Juu ya Balkoni hiyo walionekana makardinali wawili waliokuwa kwenye upande wa Papa Kardinali Dominique Mamberti na Fernando Vérgez Alzaga, Rais Mstaafu wa Mji wa Vatican na Askofu Mkuu Diego Ravelli, Mshereheshaji wa Maadhimisho ya Kiliturujia ya Kipapa, na ambaye, Baba Mtakatifu alimwomba asome Ujumbe wa Pasaka akiwaeleza waamini waliokuwa katika uwanja. Ufuatao ni ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Roma na Ulimwengu mzima(URBI ET ORBI):
Kristo amefufuka, aleluya! Kaka na dada, Heri ya Pasaka! Leo Aleluya hatimaye inasikika katika Kanisa, inasikika kutoka mdomo hadi mdomo, kutoka moyo hadi moyo, na uimbaji wake unawafanya watu wa Mungu ulimwenguni kote kulia kwa furaha. Kutoka kwenye kaburi tupu huko Yerusalemu linakuja tangazo ambalo halijasikika: Yesu, Msulubiwa, "hayupo hapa, lakini amefufuka" (Lk 24: 6). Hayupo kaburini, yu hai! Upendo umeshinda chuki. Nuru imeshinda giza. Ukweli umeshinda uongo. Msamaha umeshinda kulipiza kisasi. Uovu haujatoweka katika historia yetu, utabaki hadi mwisho, lakini hauna mamlaka tena, hauna nguvu tena juu ya wale wanaokaribisha neema ya siku hii. Kaka na dada na hasa nyinyi wenye majonzi na uchungu, kilio chenu cha kimya kimya kimesikika, machozi yenu yamekusanywa, hakuna yaliyopotea! Katika mateso na kifo cha Yesu, Mungu alichukua maovu yote ya ulimwengu na kwa huruma yake isiyo na kikomo akayashinda: Ameondoa kiburi cha kishetani ambacho kinatia sumu mioyoni mwa mwanadamu na kupanda vurugu na ufisadi kila mahali. Mwanakondoo wa Mungu ameshinda! Kwa sababu hiyo leo tunasema: "Kristo, tumaini langu, amefufuka!" (sekwensia ya Pasaka). Ndiyo, ufufuko wa Yesu ndio msingi wa tumaini: kuanzia tukio hili, matumaini si udanganyifu tena. Hapana. Shukrani kwa Kristo aliyesulubiwa na kufufuka, tumaini halikatishi tamaa! Spes non confundit! (cfr Rm 5,5). (taz. Rum 5:5). Na si matumaini ya kukwepa, bali ni changamoto; sio kutengwa, lakini kuwabika.
Wale wanaomtumaini Mungu huweka mikono yao dhaifu katika mkono wake mkuu na wenye nguvu, wanajiachia kuinuliwa na kuanza safari yao: pamoja na Yesu mfufuka wanakuwa mahujaji wa matumaini, mashuhuda wa ushindi wa Upendo, wa nguvu ya Uzima iliyonyang'anywa silaha. Kristo amefufuka! Tangazo hili lina maana nzima ya kuwepo kwetu, ambayo haifanywi kwa ajili ya kifo bali kwa ajili ya maisha. Pasaka ni sherehe ya maisha! Mungu alituumba kwa ajili ya uzima na anataka wanadamu wafufuliwe! Machoni mwake kila maisha ni ya thamani! kuanzia na yule mtoto aliye tumboni mwa mama yake, kama ilivyo wazee au wagonjwa, wanaonwa kama idadi katika nchi nyingi na kuwa watu wa kutupwa. Ni kiasi gani cha vifo tunachokiona kila siku katika migogoro mingi inayoathiri sehemu mbalimbali za dunia! Ni ukatili kiasi gani tunaona mara nyingi hata katika familia, dhidi ya wanawake au watoto! Ni dharau kiasi gani wakati mwingine huhisiwa kwa wanyonge, waliotengwa, na wahamiaji! Katika siku hii, ningependa turudi kwenye tumaini na imani kwa wengine, hata kwa wale ambao hawako karibu nasi au wanaotoka nchi za mbali na mila na desturi, njia za maisha, mawazo, na tabia tofauti na zile zinazojulikana zaidi kwetu, kwa sababu sisi sote ni watoto wa Mungu!
Natamani turudi nyuma katika matumaini kwamba amani inawezekana! Kutoka katika Kaburi Takatifu, Kanisa la Ufufuko, ambapo Pasaka ya mwaka huu inaadhimishwa siku hiyo hiyo na Wakatoliki na Waorthodox mwanga wa amani uangaze juu ya Nchi Takatifu yote na juu ya ulimwengu wote. Niko karibu na mateso ya Wakristo huko Palestina na Israeli, pamoja na watu wote wa Israeli na watu wote wa Palestina. Kuna wasiwasi kuhusu hali ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi ambayo inaenea duniani kote. Wakati huo huo, mawazo yangu yanawaendea watu na hasa jumuiya ya Kikristo ya Gaza, ambako mzozo wa kutisha unaendelea kuzalisha kifo na uharibifu na kusababisha hali mbaya ya kibinadamu. Ninatoa wito kwa pande zinazopigana: zikomeshe moto, waachilie mateka na wape msaada watu, ambao wana njaa na wanaotamani mustakabali wa amani! Tuziombee jumuiya za Kikristo huko Lebanon na Syria ambao, wakati nchi ya mwisho inakabiliwa na mabadiliko tete katika historia yake, wanatamani utulivu na ushiriki katika hatima ya mataifa yao. Ninalihimiza Kanisa zima kusindikiza kwa umakini na sala kwa Wakristo wapendwa wa Mashariki ya Kati. Pia ninatoa wazo maalum kwa watu wa Yemen, ambao wanakabiliwa na mojawapo ya majanga ya kibinadamu "ya muda mrefu" duniani kutokana na vita, na ninamwalika kila mtu kutafuta suluhisho kupitia mazungumzo yenye kujenga.
Kristo Mfufuka amimine zawadi ya Pasaka ya amani kwa Ukraine inayoteswa na kuwatia moyo watendaji wote wanaohusika kuendeleza juhudi zao za kufikia amani ya haki na ya kudumu. Katika siku hii ya sherehe, hebu tufikirie kuhusu Caucasus ya Kusini na tuombee utiaji saini wa mapema na utekelezaji wa Mkataba madhubuti wa Amani kati ya Armenia na Azabajani, ambao utaleta upatanisho unaotarajiwa sana katika Kanda. Na mwanga wa Pasaka utie msukumo maazimio ya maelewano katika eneo la Balkan Magharibi na kusaidia watendaji wa kisiasa katika kufanya kazi ili kuepusha kuongezeka kwa mivutano na migogoro, pamoja na washirika katika Kanda katika kukataa tabia hatari na zinazovuruga. Kristo Mfufuka, tumaini letu, awape amani na faraja Waafrika ambao ni wahanga wa ghasia na migogoro, hasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan na Sudan Kusini, na awasaidie wale wanaoteseka kwa sababu ya mivutano katika Sahel, Pembe ya Afrika na Ukanda wa Maziwa Makuu, pamoja na Wakristo ambao katika sehemu nyingi hawawezi kukiri imani yao kwa uhuru. Hakuna amani inayowezekana pale ambapo hakuna uhuru wa kidini au pale ambapo hakuna uhuru wa mawazo na usemi na kuheshimu maoni ya wengine. Hakuna amani inayowezekana bila kupokonywa silaha kweli! Haja ambayo kila mtu anapaswa kujitolea kwa utetezi wake haiwezi kubadilishwa kuwa mashindano ya jumla ya silaha. Nuru ya Pasaka inatutaka tuvunje vizuizi vinavyoleta migawanyiko na matokeo mabaya ya kisiasa na kiuchumi. Inatuhimiza kutunzana, kuongeza mshikamano wa pamoja, kufanya kazi ya kukuza maendeleo fungamani ya kila binadamu.
Katika wakati huu, msaada wetu usikose kwa watu wa Birmania( Myanmar) ambao tayari wameteswa na miaka ya vita vya silaha, ambao wanakabiliwa na ujasiri na uvumilivu matokeo ya tetemeko la ardhi la Sagaing, sababu ya vifo vya maelfu ya watu na chanzo cha mateso kwa wengi walionusurika, miongoni mwao mayatima na wazee. Tunawaombea waathirika na wapendwa wao na tunawashukuru kutoka ndani ya kina cha mioyo yetu wanaojitolea wakarimu ambao wanafanya shughuli za uokoaji. Tangazo la kusitishwa kwa mapigano na watendaji mbalimbali nchini humo ni ishara ya matumaini kwa Myanmar yote. Ninatoa wito kwa wale wote duniani wenye majukumu ya kisiasa kutokubali mantiki ya hofu inayofungwa, bali watumie rasilimali zilizopo kusaidia wahitaji, kupambana na njaa na kukuza mipango ya kukuza maendeleo. Hizi ndizo "silaha" za amani: zile zinazojenga siku zijazo, badala ya kupanda kifo! Kanuni ya ubinadamu isipotee kamwe kama msingi wa matendo yetu ya kila siku. Kwa kukabiliwa na ukatili wa migogoro ambayo inahusisha raia wasio na ulinzi, kushambulia shule na hospitali na wafanyakazi wa kibinadamu, hatuwezi kumudu kusahau kwamba sio walengwa wanaopigwa, lakini watu wenye roho na hadhi.
Na katika mwaka huu wa Jubilei, Pasaka pia iwe ni siku kuu ya kuwaachilia wafungwa wa vita na wafungwa wa kisiasa! Ndugu wapendwa, katika Pasaka ya Bwana, kifo na uzima vilikabiliana katika pambano la ajabu, lakini Bwana sasa anaishi milele (tazama Sekwensia ya Pasaka) na anatia ndani yetu uhakika kwamba sisi pia tumeitwa kushiriki katika maisha yasiyo na mwisho, ambayo mapigano ya silaha na mwangwi wa kifo hautasikika tena. Hebu na tujikabidhi kwake yeye peke yake awezaye kufanya mambo yote kuwa mapya (rej. Ufu 21:5)! Pasaka njema kwa wote!