Tafuta

Kardinali Leonardo Sandri, tarehe 30 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maombolezo ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa wahudumu wa Kikanisa cha Kipapa. Kardinali Leonardo Sandri, tarehe 30 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maombolezo ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa wahudumu wa Kikanisa cha Kipapa.   (@Vatican Media)

Maombolezo ya Kifo cha Papa Francisko: Wahudumu Wa Kikanisa Cha Kipapa

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ambaye pia ni Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinali, tarehe 30 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maombolezo ya Hayati Papa Francisko kwa wahudumu wa Kikanisa cha Kipaa. Anasema, Fumbo la Pasaka ni utimilifu wa Fumbo la Umwilisho kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican “Sacrum novendiale, Novendia” ni kipindi cha siku tisa za maombolezo kinachofuatia kifo cha Baba Mtakatifu na kuanza mara baada ya mazishi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na tarehe yake hupangwa na Baraza la Makardinali na maadhimisho haya yanafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican, Dominika tarehe 27 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya pili ya Novendia, maalum kwa wafanyakazi pamoja na raia wanaoishi mjini Vatican. Kardinali Parolin katika mahubiri yake amegusia kuhusu: Majonzi makubwa katika kipindi hiki cha maombolezo ya Baba Mtakatifu Francisko, lakini jambo la msingi ni furaha ya Pasaka; changamoto mamboleo katika maisha ya vijana, lakini wanapaswa kujikita katika upendo ambao hustahimili yote. Upendo wenye huruma ni kiini cha mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo na kwamba, Kanisa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu.

Maombolezo ya kifo cha Baba Mtakatifu Francisko siku ya tano
Maombolezo ya kifo cha Baba Mtakatifu Francisko siku ya tano   (@Vatican Media)

Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, Jumatatu jioni tarehe 28 Aprili 2025 akiwa ameungana na waamini wa Jimbo kuu la Roma, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya Tatu ya Novendia. Katika mahubiri yake amegusia majonzi makubwa kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma ambao wanaomboleza kwa kuondokewa na Mchungaji wao mkuu, sasa wamekuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, huyu ni mchungaji aliyewapenda sana kondoo wake, lakini wakumbuke kwamba, Kristo Yesu ndiye mchungaji wa kweli, aliyeleta mageuzi katika historia ya ukombozi wa mwanadamu, anatambua uzito wa mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu. Kipindi hiki cha majonzi ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kwani maisha yana nguvu zaidi ya kifo.

Kardinali Leonardo Sandri akiongoza Misa ya Maombolezo
Kardinali Leonardo Sandri akiongoza Misa ya Maombolezo   (@Vatican Media)

Kardinali Mauro Gambetti, O.F.M. Conv., Makamu Askofu mkuu mjini Vatican, akiwa ameungana na wahudumu wa Makanisa makuu Jimbo kuu la Roma, Jumanne jioni tarehe 29 Aprili 2025 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Katika mahubiri yake, Kardinali Gambetti anasema, Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, toka huko, Kristo Yesu atakuja kuwahukumu wazima na wafu na Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Yeye ni Bwana wa ulimwengu na wa historia. Ndani yake historia ya mwanadamu na pia kazi nzima ya uumbaji hujumlishwa na kutimilizwa kwa namna iliyo bora kabisa. Ukombozi ni chemchemi ya mamlaka ya Kristo Yesu ambayo anayatekeleza kwa nguvu ya Roho Mtakatifu juu ya Kanisa. Manabii na hatimaye, Yohane Mbatizaji alitangaza katika mafundisho yake kuhusu hukumu ya siku ya mwisho. Hapo matendo ya kila mmoja yatafunuliwa pamoja na siri za nyoyo za watu. Kumbe, huu ni wakati muafaka wa kutumia vyema neema ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo kwani hiki ndicho kitakachokuwa ni kipimo Siku ya hukumu ya mwisho.

Watu wa Mungu wakihudhuria Misa ya Maombolezo ya Papa Francisko
Watu wa Mungu wakihudhuria Misa ya Maombolezo ya Papa Francisko   (@Vatican Media)

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ambaye pia ni Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinali, tarehe 30 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maombolezo ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa wahudumu wa Kikanisa cha Kipapa. Katika mahubiri yake anasema, Fumbo la Pasaka ni utimilifu wa Fumbo la Umwilisho kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu amewakirimia wanadamu dunia mpya inayoambata wokovu ulioletwa na Kristo Yesu. Huu ndio mwanga unaowaangaza watakatifu na mashuhuda wa imani walioenea sehemu mbalimbali za dunia. Fumbo la Pasaka ni sababu na kiini cha imani, furaha na matumaini ya Wakristo hapa duniani kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kuwakirimia maisha ya uzima wa milele, mwaliko wa kudumisha upendo.

Watu wa Mungu wakihudhuria Ibada ya Maombolezo.
Watu wa Mungu wakihudhuria Ibada ya Maombolezo.

Kwa njia ya huruma na upendo wa Mungu, waamini wamepewa matumaini mapya. Ufufuko wa Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha kuu “Gaudium magnum” kama itakavyokuwa baada ya Kanisa kumpata Papa mpya. “Sacrum novendiale, Novendia”: Kipindi cha siku tisa za maombolezo kinachofuatia kifo cha Baba Mtakatifu ni muda muafaka wa kuwaimarisha waamini katika imani katika Fumbo la Pasaka. Yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu; Ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani na msamaha wa dhambi; kwa kuendelea kujikita katika ujenzi wa umoja na ushirika wa Kanisa, kwa kujiaminisha mikoni mwa Mungu. Mama Kanisa anafundisha kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma inayotekelezwa katika medani mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa. Kimsingi Khalifa wa Mtakatifu Petro ni mtumishi wa watumishi wa Mungu “Servus Servorum” ushuhuda makini uliotolewa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake: kwa kuwaosha wafungwa miguu, kuwapigia magoti viongozi wa Sudan ya Kusini na kwamba, Makardinali ni wasaidizi wa kwanza wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuwa, wao ni Mashuhuda wa kazi ya Roho Mtakatifu. Kwa kushukiwa na Roho Mtakatifu, waamini wanaitwa na kutumwa kwenda sehemu mbalimbali za Ulimwengu kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Novendia ni kipindi cha siku tisa za maombolezo ya Papa
Novendia ni kipindi cha siku tisa za maombolezo ya Papa   (@Vatican Media)

Wakristo wote kunako mwaka 2033 wataadhimisha Jubilei ya Miaka Elfu mbili ya Ukombozi unaokita mizizi yake katika: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kukuza na kuimarisha: imani, matumaini na mapendo. Waamini wanahimizwa kutangaza na kushuhudia ufufuko wa Kristo Yesu. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ambaye pia ni Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinali, mwishoni mwa mahubiri yake, amemweka Hayati Baba Mtakatifu Francisko chini ya ulinzi na tunza ya Bikira  Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, ili aendelee kumwombea Hayati Baba Mtaklatifu Francisko, aliyeonesha Ibada ya hali ya juu kabisa lakini kwa sasa anapumzika kwenye usingizi wa amani, huku akiwa na tumaini la maisha na uzima wa milele kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu.

Kardinali Sandri
01 Mei 2025, 14:35