Tafuta

Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga tarehe 12 Aprili 2025 amefanya kumbukizi ya Miaka 10 tangu alipoteuliwa kuwa Askofu. Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga tarehe 12 Aprili 2025 amefanya kumbukizi ya Miaka 10 tangu alipoteuliwa kuwa Askofu. 

Askofu Liberatus Sangu Jimbo Katoliki la Shinyanga: Miaka 10 ya Huduma!

Baada ya kuanza utume wake katika Jimbo la Shinyanga akiongozwa na Kauli mbiu yake ya kiaskofu: “Tunda la roho ni upendo” amefanya juhudi za kuchochea moyo wa imani, matumaini na mapendo kwa waamini pamoja na kuwawezesha kutambua umuhimu wa kulitegemeza Kanisa, hatua ambayo imesaidia sana Jimbo kustawi kiroho na kimiundombinu; kukuza na kudumisha miito mitakatifu; maboresho ya huduma za kijamii: Ulinzi wa Mali ya Kanisa!

Na Mwandishi Maalum, - Jimbo Katoliki Shinyanga, Tanzania.

Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga tarehe 12 Aprili 2025 amefanya kumbukizi ya Miaka 10 tangu alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, akipewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifu watu wa Mungu. Askofu Sangu ambaye ni Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga, aliwekwa wakfu na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga mnamo tarehe 12.04.2015, baada ya Jimbo la Shinyanga kuwa wazi kwa takribani miaka miwili, kufuatia kifo cha aliyekuwa Askofu wa tatu wa Jimbo la Shinyanga Hayati Aloysius Balina, aliyefariki dunia tarehe 6 Novemba 2012.Itakumbukwa kwamba, Askofu Liberatus Sangu alizaliwa kunako tarehe 19 Februari 1963, Kijijini Mwazye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi kwenye Seminari kuu la Kibosho, Jimbo Katoliki Moshi na Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam, akapadrishwa kunako tarehe 9 Julai 1994. Katika maisha na utume wake kama Padre, Askofu Sangu aliwahi kuwa: Mlezi wa Seminari ndogo ya Kaengesa, Jimbo Katoliki la Sumbawanga kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 1995. Akateuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Matai kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 1996. Kati ya Mwaka 1996 hadi mwaka 1999 alikuwa mjini Roma kwa masomo ya juu na hivyo kujipatia shahada ya Uzamili katika taalimungu ya Sakramenti za Kanisa, kutoka katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Anselmi, kilichoko mjini Roma.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania

Kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2000, aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Parokia ya Mwazye. Kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2007 akateuliwa kuwa ni Mkurugenzi wa Miito Jimbo Katoliki la Sumbawanga; Mlezi katika mwaka wa malezi na Mkurugenzi wa Utume wa Vijana, Jimbo Katoliki Sumbawanga. Kunako mwaka 2007 hadi mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Paroko wa muda Parokiani Sopa. Kuanzia mwaka 2008 hadi uteuzi wake, amekuwa akitekeleza utume wake kama Afisa mwandamizi, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu mjini Vatican. Askofu Sangu ambaye ni mzaliwa wa Jimbo la Sumbawanga, aliteuliwa kuwa Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga mnamo tarehe 02.02.2015. Baada ya kuanza utume wake katika Jimbo la Shinyanga akiongozwa na Kauli mbiu yake ya Kiaskofu: “Tunda la roho ni upendo” amefanya juhudi kubwa za kuchochea moyo wa imani, matumaini na mapendo kwa waamini pamoja na kuwawezesha kutambua umuhimu wa kulitegemeza Kanisa, hatua ambayo imesaidia sana Jimbo Katoliki la Shinyanga kustawi kiroho na kimiundombinu. Baada ya kuanza utume wake jimboni Shinyanga, Askofu Sangu aliweka mkakati maalum wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu akiongonzwa na kauli mbiu aliyoiasisi ya “tusimame imara katika imani” kwa kuhakikisha anayafikia maeneo yote ya Jimbo, mijini na vijijini, akijielekeza zaidi kwenye maeneo ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele kutokana na changamoto mbalimbali za kijamii na hivyo kusababisha yakose huduma muhimu ikiwemo za kiroho. Maeneo hayo ni pamoja Gambosi (Gamboshi) kijiji maarufufu kilichopo wilayani Bariadi mkoani Simiyu na Bukundi wilayani Meatu mkoani Simiyu ambako wanaishi wafugaji wa jamii ya Kitaturu.

Askofu Sangu Uteuzi 2 Februari 2015
Askofu Sangu Uteuzi 2 Februari 2015   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Katika kuhakikisha watu hao wanafikiwa na huduma za kiroho, Askofu Sangu alianzisha Parokia mpya ya Ngulyati kwa ajili ya watu wa Gambosi na maeneo mengine yanayozunguka eneo hilo, ambapo katika kuwafikia watu wa jamii ya Kitaturu alianzisha Parokia mpya ya Bukundi iliyopo karibu na maeneo wanayoishi. Parokia hizo zimeendelea kukua ambapo kwa upande wa eneo la Gambosi (Parokia ya Ngulyati) imeanzishwa shule maalum ya msingi ya mchepuo wa kiingereza (English medium) ambayo imetoa fursa ya kupata elimu bora kwa watoto wa eneo hilo na hasa wanaotoka katika familia maskini. Askofu Sangu pia ameanzisha kituo cha hija ya Imani katika Kanisa la Mtakatifu Mikaeli Malaika mkuu Parokia ya Sayusayu ambalo ni la kwanza kujengwa katika Jimbo la Shinyanga, lililoanzishwa mnamo mwaka 1928. Watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo la Shinyanga wanakwenda kufanya hija na tafakari katika Kanisa hilo, ambamo umewekwa Msalaba wa Jubilei ya miaka 2,000 ya Ukristo. Halikadhalika amekiendeleza Kituo cha Jimbo cha Hija ya Huruma ya Mungu kilichopo katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Parokia ya Nkololo Wilayani Bariadi mkoani Simiyu, ambapo kila mwaka waamini kutoka sehemu mbalimbali za Jimbo hukutana kwa hija na kufanya mafungo na ibada ambavyo huhitimishwa kwa Ibada ya Misa ya Takatifu.

WAWATA Shinyanga Inawategemeza Watawa Jimboni humo
WAWATA Shinyanga Inawategemeza Watawa Jimboni humo

KUHUSU KUSOGEZA HUDUMA ZA KIROHO KWA WATU: Kupitia mpango maalum aliouanzisha wa kusogeza huduma za kiroho kwa watu, ndani ya kipindi chake cha miaka 10 ya Uaskofu amefanikiwa kuanzisha Parokia mpya jumla ya 14 na kulifanya Jimbo la Shinyanga kuwa na Jumla ya Parokia 40 badala ya 26 alizozikuta. Parokia mpya ambazo zimeanzishwa na Askofu Sangu ni: Ngulyati, Bukundi, Old Shinyanga, Nindo, Ndala, Kitangili, Lubaga, Maganzo, Mhunze, Mtakatifu Luka-Bariadi, Luguru, Shishiyu, Lagangabilili na Ndembezi. Aidha, ametangaza Parokia nyingine teule zaidi ya 5 ambazo baadhi yake ziko kwenye mchakato wa kufanywa kuwa Parokia kamili na nyingine zinaendelea kufanyiwa upembuzi. Parokia teule ambazo amezitangaza ni pamoja na: Imalaseko ambayo kwa sasa ni sehemu ya Parokia ya Ng’wanhuzi, Nyashimo ambayo kwa sasa ni sehemu ya Parokia ya Ng’wanangi, Masanwa ambayo kwa sasa ni sehemu ya Parokia ya Nyalikungu, Lyamidati ambayo kwa sasa ni sehemu ya Parokia ya Bugisi na Mwakitolyo aliyoitangaza hivi juzi ambayo kwa sasa ni sehemu ya Parokia ya Salawe. Pia katika kufanikisha mpango wa kusogeza huduma za kiroho kwa watu, uongozi wa Jimbo na Parokia umeendelea kununua maeneo kwa ajili ya kujenga Makanisa ya kudumu ikiwemo kuyapanua na kuyaboresha yaliyokuwepo hapo awali. Aidha kupitia mpango huo, Askofu Sangu amewasilisha pendekezo la kuanzishwa kwa Jimbo jipya la Bariadi ambalo litapatikana kwa kugawanywa kwa Jimbo la Shinyanga, ambapo kwa sasa mchakato wa kuanzishwa kwa Jimbo hilo unaendelea chini ya Askofu wa Roma Baba Mtakatifu Francisko. Kwa kutambua kwamba suala la kusogeza huduma za kiroho kwa watu litahitaji watenda kazi wa kutosha, Askofu Sangu ametoa hamasa kwa vijana ambapo wengi wameitikia wito wa Upadre. Mpaka sasa Jimbo la Shinyanga lina jumla ya Mafrateri 100 ambao baadhi yao wako mwaka wa uchungaji mkubwa na wengine wako kwenye hatua mbalimbali za malezi Seminarini. Katika kipindi cha mwaka 2015 kurudi nyuma Jimbo la Shinyanga lilikuwa na Mafrateri wasiozidi 20. Idadi ya Mapadre wazalendo nayo inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2024, Jimbo la Katoliki la Shinyanga liliweka kumbukumbu katika historia yake kwa kupata Mapadre wapya 11 kwa mkupuo, waliopewa daraja hilo mnamo mwezi Julai.

Katika kipindi cha miaka kumi, miito imeongezeka maradufu
Katika kipindi cha miaka kumi, miito imeongezeka maradufu   (Jugo Media)

KUHUSU KULITEGEMEZA KANISA MAHALIA: Baada ya Askofu Sangu kuchochea moyo wa imani, matumaini na mapendo kwa waamini na kutambua umuhimu wa kulitegemeza Kanisa, wanajitoa na kushiriki katika kufanikisha shughuli mbalimbali za ustawi na maendeleo ya Kanisa ikiwemo kujenga Makanisa ya kudumu na ya kisasa kwenye vigango na Parokia zao, wanawategemeza Mapadre wao na kulitegemeza Jimbo bila kusubiri misaada kutoka kwa watu wa nje kama ilivyokuwa hapo awali. Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Jimbo Katoliki Shinyanga (WAWATA) nao wameendelea kumuunga mkono Askofu Sangu kwa kuwategemeza kwa vitu mbalimbali walelewa wa Shirika la Watawa wa kike la kijimbo la Bikra Maria Mama wa huruma. Kuhusu kuwaendeleza Mapadre Kielimu. Katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake, Askofu Sangu amefanikiwa kuwapeleka kujiendeleza kielimu Mapadre zaidi ya 15 katika vyuo mbalimbali vya Elimu ya juu vilivyopo ndani na nje ya nchi, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu, wakimtangaza Kristo huku wakiwa na mang’amuzi mazuri na ya kina juu ya kumsaidia mwanadamu kutokana na changamoto zinazomkabili kiroho na kimwili. Maboresho ya huduma za kijamii: Askofu Sangu ameendelea kuboresha miradi ya huduma kwa jamii ikiwemo elimu na Afya, ambapo katika upande wa Elimu amewatuma Mapadre wenye Elimu na sifa kwenda kusimamia Shule za Sekondari zinazomilikiwa na kuendeshwa na Jimbo Katoliki la Shinyanga pamoja na kuelekeza kila Parokia mpya inayoanzishwa lazima iwe na shule hasa ya watoto wadogo ili kuwaandaa vizuri kielimu, kimaadili na kiutu! Askofu Sangu ameweka usimamizi mzuri katika Seminari ndogo ya Shanwa iliyopo mjini Maswa mkoani Simiyu, ambayo inaendelea kuwa moja ya shule bora zaidi katika mkoa wa Simiyu. Aidha, katika miradi ya Afya ameendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuboresha huduma za afya zinazotolewa na Jimbo, ambao ni pamoja na Shirika na Madaktari na Afrika (CUAMM) linalohudumia watu mbalimbali ikiwemo watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Askofu Sangu pia anaendelea na mchakato wa kukiwezesha kituo cha afya Ngokolo kutoa huduma za upasuaji pamoja na kupata vifaa tiba vya kisasa zaidi.

Maboresho ya Radio Faraja Shinyanga Yanaendelea
Maboresho ya Radio Faraja Shinyanga Yanaendelea

RADIO FARAJA: Katika kuhakikisha Radio Faraja inayomilikiwa na Jimbo inakuwa na uwezo mkubwa wa kusaidia shughuli za Uinjilishaji, ameanzisha mpango maalum wa kuitegemeza Redio ili isikwame kutekeleza majukumu yake kutokana na changamoto ya kifedha. Kwa sasa Radio Faraja iko kwenye mchakato wa kukusanya fedha ili kuboresha miundombinu, kupanua wigo wa matangazo yake na kununua vifaa vya kisasa. Askofu Sangu ametilia mkazo kwa Radio Faraja kuhakikisha vipindi vyake vinaisaidia jamii katika mazingira yote ya kiroho na kijamii. Maboresho ya miundo mbinu: Askofu Sangu ameboresha miundombinu ya Makao makuu ya Jimbo na Kanisa kuu, pamoja na kuanzisha ujenzi wa Hosteli mpya ya Mapadre ambao uko katika hatua za mwisho. Askofu Sangu pia ameanzisha shirika jipya la watawa wa kike la kijimbo la Bikra Maria mama wa Huruma, ambalo kwa sasa linalelewa na Masista wa shirika la Bikra Maria Malkia wa mitume toka Jimbo kuu la Mbeya. Watawa wa Shirika la Jimbo la Shinyanga ambao tayari wamefunga nadhiri kwa sasa wanafanya utume katika Parokia mbalimbali za Jimbo la Shinyanga na wengine wanajiendeleza kielimu. Usimamizi na Ulinzi wa Mali za Kanisa: Pamoja na Jimbo kuendelea kununua ardhi mpya kupitia Maparoko walioko kwenye Parokia, Askofu Sangu ameweka mkazo katika usimamizi wa mali za Kanisa na hasa ardhi iliyokuwa imeanza kuvamiwa na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu ikiwemo wasiojua vizuri mipaka ya Kanisa hasa baada ya wazazi wao kufariki. Malezi na makuzi kwa vijana: Katika uongozi wake, Askofu Sangu kwa kushirikiana na Mapadre ametilia mkazo na kusisitiza juu ya malezi kwa vijana na watoto kuanzia ngazi ya familia na kupitia vyama vyao vya kitume hatua ambayo imechangia kijana kutoka Jimbo la Shinyanga kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Vijana Wakatoliki wafanyakazi (VIWAWA) wa Kanda na Taifa.

Askofu Sangu akisalimiana na Rais Mstaafu J. Kikwete
Askofu Sangu akisalimiana na Rais Mstaafu J. Kikwete

KUHUSU AMANI UMOJA NA MAADILI NA UTU WEMA: Askofu Sangu ameendelea kuwa mjumbe wa amani kwa kutoa mafundisho yanayohamasisha amani na umoja ndani ya jamii na taifa, akisisitiza viongozi kutenda haki na kuacha ubinafsi na uroho wa madaraka mambo ambayo yanasababisha hali ya chuki, fitina na mafarakano ikiwemo vita vya wenyewe kwa wenyewe. Msisitizo wake kwa watu wote wa Mungu ni kujenga moyo wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa Mungu na jirani, kuacha kutumia shida za wengine kujinufaisha, kuwahurumia wengine na kuwajali na kuwa faraja kwa watu wenye shida. Aidha, msisitizo wake kwa Radio Faraja ambayo inamilikiwa na kuendeshwa na Jimbo Katoliki la Shinyanga ni kuendelea kuwa kiungo cha umoja, upendo na mshikamano kwa watu wa kabila, itikadi na dini zote, pamoja na kuhakikisha inandaa vipindi vyenye maaudhui ya kuijenga jamii ikiwemo kupinga mambo yote yasiyofaa ikiwemo, ukatili dhidi ya binadamu na hasa kwa wanawake na watoto. Askofu Sangu daima amekuwa mkali kwenye suala la ndoa za jinsia moja huku akisisitiza kuwa, Afrika kamwe isikubali kupokea na kujiingiza katika jambo hilo iwe ni kwa ushawishi wa fedha au kwa namna yoyote ile, kwa vile licha ya kwenda kinyume na mpango ya Mwenyezi Mungu, kanuni maadili na utu wema linavuruga na kuua kabisa tunu ya maisha ya ndoa ambayo ndiyo msingi wa familia. Anapotimiza miaka 10 ya Uaskofu, Askofu Sangu anawaomba waamini wa Jimbo la Shinyanga waendelee kumwombea kwa Mungu bila kuchoka, ili aweze kutekeleza vizuri na kwa uaminifu utume aliokabidhiwa na Mungu kupitia nafsi ya Baba Mtakatifu, akizingatia mfano wa Kristo aliye mchungaji mwema.

Askofu Sangu
12 Aprili 2025, 17:26