Tafuta

Wanafunzi na mavazi yao yao ya Chuo. Wanafunzi na mavazi yao yao ya Chuo. 

3 Mei 2025,Misa ya Ushemasi Vatican:Yesu alihudumu ili nasi tutumikiane!

“Nimechagua maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo kutoka katika Injili ya Marko 10:45 kuwa dira yangu ya utumishi:“Maana Mwana wa mtu hakuja kutumikiwa,bali kutumika na kutoa nafsi yake kuwa fidia kwa wengi."Ndivyo anasema Frateli Theogenes Petro Madushi,mseminari wa Chuo Kikuu cha Kipapa atakayepewa daraja la ushemasi pamoja na wengine 11 kutoka pande za dunia mikononi mwa Kardinali Tagle katika Basilika ya Mtakatifu Petro mjini Vatican,Mei 3.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Jumamosi tarehe 3 Mei 2025 katika mwaka wa Jubilei Kuu ya 2025, Basilika ya Mtakatifu Petro mjini Vatican, saa 12.00 jioni masaa ya Ulaya, ikiwa ni saa 1 za Afrika Mashariki na Kati, kutakuwa na maadhimisho ya Misa takatifu ya kuwekwa kwa daraja la Ushemasi kwa mashemasi 12 kutoka sehemu mbali mbali za Dunia wanaosoma katika vyuo vikuu vya kipapa. Misa hiyo itaongozwa na Kardinali Antonio Tagle. Miongoni mwa waseminari hao, kuna wawili kutoka Tanzania. Katika fursa hiyo Vatican News, imezungumza na Fratelii Theongenes Petro Madushi, ambaye katika fursa hiyo amechagua maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo kutoka katika Injili ilivyoandikwa na Marko 10:45 kuwa kama dira ya  utumishi wake: “Maana Mwana wa mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kutoa nafsi yake kuwa fidia kwa wengi” na Mtakatifu Agustino naye kwa kuzingatia maneno hayo ya Kristo anasema: “Yesu alichukua hali ya mtumwa ili kutufanya sisi kuwa huru, alihudumu ili sisi tujifunze kutumikiana, alijinyenyekeza ili kutuinua.” Namuomba Mungu anifundishe kutumikia kwani yeye ndiye kielelezo cha utumishi.” Ni sehemu ya sentensi ambayo inatupatia mwanga juu ya huduma ya Yesu na ambayo aliacha mfano wa huduma ya mashemasi wote katika Kanisa. Ufuatayo ni ushuhuda wa maisha yake.

Hawa ni mashemasi wa tarehe 2 Mei 2024 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro
Hawa ni mashemasi wa tarehe 2 Mei 2024 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro

Ninaitwa Frateli Theogenes Petro Madushi, mseminari wa Jimbo kuu la Mwanza Tanzania. Ninasoma Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana Roma. Nilizaliwa tarehe 26 Februari 1995 nikiwa mzaliwa wa kwanza katika familia ya watoto wawili, Parokia ya Mtakatifu Bernadetta Kahangara,  Wilaya ya Magu, mkoa wa Mwanza. Baba yangu anaitwa Emanuel Sama na Mama yanngu anaitwa Angela Migozi, lakini jina lake maarufu anaitwa Edda Ndindagi, na mdogo wangu anaitwa Jovini Sama.

Maisha yangu

Nilianza elimu ya msingi mwaka 2003 na nikahitimu mwaka 2009 katika shule ya msingi Mwamanga, kata ya Mwamanga Wilaya ya Magu. Baadaye nilichaguliwa kujiunga na shule ya Sekondari kuanzia mwaka 2010 mpaka 2013 huko Mwamanga, kisha nilichaguliwa kujiunga na masomo ya A-level tangu mwaka 2014 hadi  2016 katika shule ya Secondari ya Kahororo iliyopo Wilaya ya Bukoba mjini Mkoa wa Kagera.

Maisha ya Kiroho

Nilibatizwa tarehe 26 Juni 2006 katika kigango cha Yichobela Parokia ya Kahangara jimbo Kuu la Mwanza na Padre Moses Mapela, na tarehe 28 oktoba 2006 nikapata Sakramenti ya Kipaimara mikononi mwa  Padre Nicholaus Segeja.

Safari ya wito

Katika safari ya wito, hamu ya kuwa Padre niliipata tangu nikiwa bado mdogo, hususani wakati tulipokuwa tukiudhuria misa Takatifu katika kigango cha Mwamanga ambako ndiko nimekulia, hivyo walipokuja Mapadre kwa ajili ya Misa niliguswa sana hasa  namna walivyokuwa wakihubiri na kuimba zile sala na prefasio. Kwa sababu hatukuwa tunapata Misa mara kwa mara hivyo Mapadre walipokuwa wanakuja ilikuwa kama sherehe, basi taratibu nilianza nami kutamani kuwa nami siku moja nifanye kama Padre anavyofanya, na kiukweli nyumbani nilikuwa naigiza jinsi Padre anavyokuwa anaongoza Misa. Pia malezi ya pale nyumbani yalichochea kukua kwa wito wangu kwa sababu kila siku jioni tulikuwa tunasali pamoja, familia yangu na familia jirani ambazo  tulikuwa marafiki,  uliokua hadi kama udugu  na ninamkumbuka rafiki wa mama yangu Mwalimu Dafroza Thomas na familia yake, hivyo walitupatia nafasi sisi watoto kuongoza sala za jioni na kusali rozari takatifu, ninawashukuru sana. Na kwa kuwa nilibatizwa nikiwa ninajitambua, hivyo wito ulianza kukua zaidi na hamu iliongezeka zaidi kipindi nilipoanza mafundisho ya ubatizo, na nikawa ninakutana watu mbalimbali wa kutoka sehemu mbali mbali tuliokuwa tunafanya mafundisho pamoja. Kwani kupitia wao na Makatekista walichochea sana hamu hii ya kumtumikia Mungu, hapo ndipo pia nilianza kupata uelewa japo kidogo kuhusu wito wa Upadre.

Na kwa upande wa malezi yangu pia ya kitaaluma katika shule ya sekondari yaani O-level na A-level, licha ya kusoma katika shule za serikali,  lakini hamu yangu ya kutaka kumtumikia Mungu kama Padre haikuisha japo pia nilitamani sana kuwa Daktari wa kutibu watu na wakati huo huo kama Padre. Namshukuru Mungu sana kwani mazingira yangu ya makuzi nilijikuta kati ya watu walionisaidia kuutambua vizuri wito huu, nakumbuka hata nikiwa sekondari pale Mwamanga nilihudumu kama mwenyekiti wa TYCS, kama katekista, si tu kati ya wanafunzi wenzangu, bali hata katika kigango cha kisesa B kilichokuwa karibu na makazi yangu pindi Katekista alipokosekana. Huduma hii niliendelea nayo hata kipindi nilipokuwa kule Kahororo Bukoba, nilihudumu kama katekista pale shuleni. Haya yote yalinisaidia kukua kiroho na kukuza hamu yangu ya kuwa Padre. Namshukuru Mwenyezi Mungu hakuniacha bali alinishika mkono na kunivusha hata sehemu nilizoona kuwa sitaweza kuvuka.

Baada ya masomo ya A-level niliamua kujiunga moja kwa moja na nyumba ya malezi, ambapo  nilipokelewa na mkurugenzi wangu wa miito Jimbo kuu la Mwanza Padre Frances Mtema kule Parokiani Kirumba, hapo sasa safari yangu ya wito ikaanza rasmi mnamno mwaka 2016. Mwaka huo huo mwezi oktoba nilitumwa kuanza masomo ya falsafa katika Seminari kuu ya Makatifu  Agostino, huko Peramiho  Jimbo Kuu Katoliki la Songea na mwaka 2019 nikamaliza masomo ya falsafa na kuanza masomo ya Taalimungu katika Seminari hiyo hiyo kuanzia Oktoba 2019 mpaka  Februari 2021, ambapo Baba Askofu Mkuu Renatus Nkwande alinituma kuja huku Roma kuendelea na masoma na malezi katika Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana na Urbano ambapo nipo hadi sasa nikiendelea na masoma ya Uzamili katika Mafundisho Tanzu ya  Kanisa nikiwa mwaka wa kwanza.

Daraja la Ushemasi

Ninapenda kumshukuru Mungu hasa zaidi ninapojiandaa kupokea Daraja Takatifu ya Ushemasi hapo tarehe 3 Mei 2025 katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei. Ni neema ya pekee ambayo Mapenzi yake Mungu amependa iwe hivyo. Ni furaha kubwa kwangu na ninaomba Mwenyezi Mungu akikamilishe kile alichokianzisha ndani mwangu.

Mafunzo ya maisha

Katika safari hii ya wito nimejifunza kuwa Padre ni sadaka; ni kuwa Ekaristi na hivyo basi kama Ekaristi inavyomegwa ndivyo yalivyo maisha ya Padre. Ninapoelekea kuwekwa katika ngazi ya kwanza ya Upadre, yaani ushemasi nalitambua hilo kuwa maisha yangu ni sadaka, na hiyo ninamuomba Mungu anipokee jinsi nilivyo. Ndiyo maana nimechagua maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo kutoka katika Injili ilivyoandikwa na Marko 10:45 kuwa kama dira yangu katika utumishi huu: “Maana Mwana wa mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kutoa nafsi yake kuwa fidia kwa wengi” na Mtakatifu Agustino naye kwa kuzingatia maneno hayo ya Kristo anasema: “Yesu alichukua hali ya mtumwa ili kutufanya sisi kuwa huru, alihudumu ili sisi tujifunze kutumikiana, alijinyenyekeza ili kutuinua.” Namuomba Mungu anifundishe kutumikia kwani yeye ndiye kielelezo cha utumishi.Kwa njia hiyo ninaomba msaada wa sala zenu ili Mungu anisimamie na kuniongoza katika kumtumikia kwa uaminifu.

Ni mengi ambayo ningeweza kusema, lakini kwa ufupi ninaomba nitoe shukrani kwa wote walionisadia na wanaoendelea kunisaidia katika malezi na makuzi yangu, wazazi wangu, walimu wangu katika shule na seminari nilizopitia katika safari hii ya malezi, ndugu zangu na marafiki zangu wote, pia na niwakaribisheni ninyi nyote Jumamosi ijayo tarehe 3  Mei 2025 katika maadhimisho ya Misa Takatifu ambamo mimi pamoja na wenzangu 11 kutoka sehemu mbali mbali za dunia tutapewa daraja ya Ushemasi katika Basilika ya Mtakatifu Petro hapa mjini Vatican.

Kardinali Tagle atatoa daraja la Ushemasi kwa mafratelli
Kardinali Tagle atatoa daraja la Ushemasi kwa mafratelli   (AFP or licensors)

Frateli Madushi hakuishia hapo, kadhalika alipenda kuwashukuru wale waliomsindikiza kwa namna ya pekee katika safari hii kwa ufupi katika lugha ya kiitaliano kwamba:

“Ringrazio tanto tutti quelli che mi aiutano e mi hanno accompagnano nel mio cammino verso il sacerdozio. Inanzitutto i miei genitori, formatori del Collegio Urbano, la famiglia di Gisele Di Liberto, Graziella Moretto, Anna Naro, Pino e Stefania Janina, Antonella, e tanti gli altri, senza dimenticare nessuno… Vi ringrazio tanto e prego sempre per voi, affinché il Signore vi benedica sempre."

Kuhusu kumbukizi ya Papa aliyeaga dunia, tarehe 21 Aprili na kuzikwa 26 Aprili 2025, Frateli madushi kwa ufupi alimkumbuka Papa Francisko kwa ukaribu wake na walio wa mwisho, kuwajali wadogo na maskini ambao mara nyingi wamesahulika katika jamii. Na alikumkubuka jinsi ambavyo mara nyingi kama waseminari wa Taasisi ya Kipapa la Urbano aliokutana nao aliwaomba  mara kadhaa wawe wazi katika kukaribishana kidugu. Kwa ujumla sura ya Baba Mtakatifu Francisko inabaki roho mwake kama ilivyo hata kwa waliowengi.

Sia lodato Gesù Cristo!Tumsifu Yesu Kristo!

Ukumbi wa Chuo Cha Kipapa cha Urbaniana
Ukumbi wa Chuo Cha Kipapa cha Urbaniana
Tupande mbegu vema, tutavuna vema
Tupande mbegu vema, tutavuna vema
Ushemasi wa mafratelli 12 katika Basilika ya Mtakatifu Petro tarehe 3 Mei 2025
30 Aprili 2025, 15:06