Papua New Guinea,mmisionari: ziara ya Papa ni alama isiyofutika!
Na Francesco Ricupero na Angella Rwezaula – Vatican.
Papa Francisko bila shaka anaacha alama ya kina sana mioyoni mwa kila mtu huko Papua New Guinea. Mi alama ambayo haitawezekana kusahaulika na ambayo itaingia katika historia kama moja ya kurasa nzuri zaidi za Kanisa katika taifa hili changa, ambalo litatimiza miaka 50 mnamo Septemba ijayo. Hivi ndivyo Padre Tomás Ravaioli, Padre mwenye umri wa miaka arobaini na tatu wa Shirika la Neno lililofanyika Mwili akizungumza na vyombo vya habari vya Vatican. Padre Tomás kutoka Buenos Aires nchini Argentina ambaye yuko kwenye utume nchini Papua New Guinea kwa karibu miaka kumi na sita, binafsi alifuatilia mchakato wa kutangazwa mtakatifu wa Katekista wa Kipapua, Peter To Rot, aliyeuawa mwaka 1945 kwa kuendeleza utume wake licha ya kupigwa marufuku iliyowekwa na Wajapan. To Rot alikufa akitetea maadili ya familia ya kitamaduni. Alikuwa na watoto watatu na mke, alipinga mitala na alilaani vikali. Huko Papua New Guinea wanamwomba kwa maombezi yake, na wanasali kwake wakiwa na furaha na shauku kwamba hivi karibuni atakuwa mtakatifu."
Lugha nyingi, makabila mengi
Kuna mambo machache sana hapa: shule, taasisi, zahanati, hospitali ndogo na vituo vya utunzaji vinafanya kazi kutokana na kazi yetu inayoungwa mkono na watu wa kawaida. Papua New Guinea ni nchi ya kuvutia, tajiri katika historia, utamaduni na mila ya kipekee. Ni nchi yenye idadi kubwa ya lugha duniani. Zaidi ya lugha 800 tofauti zinazungumzwa, ambazo zinawakilisha karibu asilimia 12 ya lugha za ulimwengu. Utamaduni ni tofauti sana, na mamia ya makabila na makabila mengi mno. Kila kabila lina desturi zake, nguo, mila na sanaa. Jiografia yake pia ni ya kuvutia, imejaa milima, volkano hai na fukwe za ajabu.
Kabla ya kufika kwa Ukristo, makabila na jumuiya za Papua New Guinea zilifuata dini za jadi, zilizozingatia imani za kimila na za kiroho. Baadhi ya imani za kiasili bado zinaendelea kuwepo katika maeneo fulani, hasa vijijini na maeneo ya mbali. Hata hivyo, leo hii wakazi wengi ni Wakristo. Ukristo ulianzishwa na wamisionari wa Uingereza, Ujerumani na Australia katika karne ya 19. Matawi makuu ya Ukristo nchini Papua New Guinea ni Ukatoliki na madhehebu mbalimbali ya Kiprotestanti, yakiwemo makanisa ya Kiinjili na makanisa ya Kianglikani.
Makanisa yalijaa kila mara
Ujumbe hapa ni wa kuvutia kweli. Kwa upande mmoja, kwa sababu ni nchi ambayo Injili ilifika hivi karibuni tu na kwa hiyo bado kuna mambo mengi ya kufanya. Kuna maeneo yasiyochafuliwa, vijiji au makabila yaliyofichwa katikati ya msitu ambao bado hawajasikia habari za Yesu au ambao wamesikia habari zake miaka michache iliyopita. Sisi kama mapadre kiukweli hatuwezi kuchoka kwa sababu tuna kazi nyingi za kufanya. Lakini pia inavutia si tu kwa sababu ni tukio bali pia kwa sababu ya mwitikio tunaopata kutoka kwa watu. Mara nyingi hutokea kwamba mapadre au wamisionari kutoka sehemu nyingine huja kututembelea hapa Papua, na wanapoona makanisa yetu yamejaa sana, wanalalamika kwa mzaha na kutuambia “laiti tungekuwa na makanisa yaliyosongamana kama yenu.”
Ujumbe wa kuiba moyo
Hii ni imani iliyo hai sana. Makanisa yanajaa watoto, wa vijana wanaokuja, lakini sio tu kwenye meza ya misa takatifu, lakini pia wanafika kuabudu Ekaristi, wanakuja kuungama kila Juma. Kwa hiyo ni imani iliyochangamka sana na kwa sisi mapadre, ambao ni wachache, kwa hiyo tuna kazi nyingi ya kufanya. Sijapata kamwe kukutana na Padre yeyote mmisionari ambaye aliwahi kulalamika au kutaka kurudi katika nchi yake, badala yeke ni kinyume kabisa. Inapotokea kwamba kuhani, ama kwa sababu za kiafya au labda kwa sababu amezeeka, inabidi arudi katika nchi yake, anafanya hivyo akilia, kwa sababu ni utume unaoiba moyo wako kweli.
Alama iliyoachwa na Papa Francisko
Kuna mambo mengi ambayo tunaweza kusema kuhusu ishara na fadhili za Papa kwa taifa hili, lakini ningependa kuorodhesha tatu tu. Awali ya yote, sisi wamisionari wa Taasisi ya Neno lilifofanyika mwili ambao tumekuwa tukifanya kazi katika jimbo la Vanimo kwa takriban miaka 30 tumejisikia kutunzwa na kulindwa hasa na upendo wake wa kibaba. Yote ilianza mnamo 2019, wakati kikundi kutoka parokia yetu kilipokwenda Roma kwa ajili ya hija kwenye kaburi la mitume. Katika hafla hiyo, Baba Mtakatifu aliwapokea katika hadhara ya faragha na kuahidi kwamba siku moja angejibu tena ziara hiyo, akija mwenyewe katika kijiji cha mbali cha Vanimo kuwatembelea. Tangu wakati huo, Papa amedumisha mawasiliano ya mara kwa mara na wamisionari katika eneo hilo, akijali si tu mahitaji ya kiroho ya waamini, bali pia mahitaji ya kimwili ya utume.
Shule inayofuatiliwa na Papa
Misheni yetu ilikuwa na shule mbili za msingi kwa watoto wa vijiji vyetu 5, lakini hatukuwa na shule ya sekondari ya kuendelea na masomo. Hili lilivunja mioyo yetu, kwa sababu ilihuzunisha kuona jinsi wengi wa watoto hao walivyoachwa bila maisha ya baadaye mara tu walipomaliza shule ya msingi, wakiwa na umri wa miaka 14 au 15. Lakini kwetu sisi ilikuwa haiwezekani kibinadamu kujenga shule ambayo inaweza kuchukua maelfu mengi ya watoto, na hivyo ilikuwa ndoto tu. Hata hivyo, ndoto hiyo ilitimia wakati Papa Francisko alipopata habari kuhusu hali hiyo na kutaka kujisimamia yeye binafsi katika ujenzi wa shule hiyo, akitafuta wafadhili kwa ajili yetu. Shule hiyo sasa inafanya kazi na watoto ambao kwa miaka mingi wameachwa bila mustakabali sasa wana mwanga mpya wa matumaini kutokana na ukarimu wa Papa.
Mtakatifu wa kwanza wa Papua New Guinea
Pili, ni lazima kukumbuka ziara ya kitume ambayo Fransisko aliifanya katika nchi yetu. Mara tu aliposhuka kwenye ndege, alimwambia Padre mmisionari ambaye alikuwa amekwenda na mahujaji mwaka 2019: "Unaona? Nilitimiza ahadi yangu. Niko hapa, kukutembelea." Ni lazima pia kusisitiza kwamba katika tukio hili alikwenda kwa utume wa Mababa wa Shirika la Neno lililofanyika Mwili na kushiriki mkutano wao binafsi na watu wa parokia yao.
Hatimaye, ishara ya tatu ya Papa Francisko kuelekea kwetu ilitokea siku chache zilizopita. Mnamo tarehe 31 Machi, Ulimwengu wote ulifurahishwa na habari kwamba mtakatifu wa kwanza wa Papua New Guinea atatangazwa kuwa mtakatifu. Bado hatujajua tarehe rasimi ya kutangazwa kwa Peter To Rot kuwa mtakatifu, lakini tunachojua ni kwamba itakuwa, kwa mara nyingine tena, hatua muhimu katika historia ya nchi hii na onyesho zaidi la upendo na upendeleo wa Baba Mtakatifu kwetu.