Tafuta

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres.  (AFP or licensors)

UN.Guterres:UN inathibitisha tena dhamira ya kupambana na ubaguzi wa rangi na kuhakikisha haki kwa wote.

Katika hafla ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Waathirika wa Utumwa na Biashara ya Watumwa ya Bahari ya Atlantiki,ikiwakumbuka mamilioni ya Waafrika walioteswa,kunyanyaswa,na kunyimwa utu wao,iadhimishwayo kila ifikapo Machi 25,Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa alielezea juu ya uhalifu uliounda dunia ya sasa,akatoa wito wa fidia na haki na ahadi ya kujenga jamii yenye usawa na heshima:“Ni wakati wa kutenda haki na kufidia waathirika wa utumwa na biashara ya watumwa."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 25 Machi, ni siku ya kimataifa ya Kumbukumbu ya Waathirika wa Utumwa na Biashara ya Watumwa ya Bahari ya Atlantiki, ambapo maadhimisho haya ya kila mwaka ni ukumbusho wa uhalifu mkubwa wa kihistoria dhidi ya ubinadamu na athari zake zinazoendelea katika jamii nyingi duniani kote. Viongozi, wanaharakati, na mashirika mbalimbali katika tukio hilo yalisisitiza umuhimu wa kutafakari, kukiri ukweli, na kuchukua hatua ili kushughulikia athari za kipindi hiki cha giza. Katika ujumbe wake wa siku hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres alisema: “Kwa zaidi ya karne nne, mamilioni ya Waafrika walitekwa kwa nguvu, kusafirishwa kwa meli hadi mataifa ya kigeni, na kufanyishwa kazi katika hali mbaya za kikatili. Biashara ya watumwa ya Bahari ya Atlantiki ilichochea ukuaji wa uchumi wa mataifa mengi ya kikoloni, huku taasisi na mashirika yakijipatia utajiri mkubwa kutokana na mateso ya watumwa.”

Mizizi ya bishara ya utumwa iliyojengwa juu ya itikadi za ubaguzi wa rangi

Kiongozi huyo wa UN alisisitiza kuwa: “Mizizi ya biashara hii ilijengwa juu ya itikadi ya ubaguzi wa rangi na dhana ya wazungungu kujiona bora kuliko wengine, ambayo athari zake zinaendelea kujidhihirisha katika mifumo ya kisasa ya kijamii, kiuchumi, na kisheria.” Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika  ujumbe wake vile vile  alisema kuwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu yanathibitisha tena dhamira yao ya kupambana na ubaguzi wa rangi na kuhakikisha haki kwa wote. Alkumbusha kuwa wakati dunia inapotafakari historia hii yenye uchungu, viongozi wanahimiza mshikamano wa kimataifa katika kujenga mustakabali wa heshima, usawa, na haki za binadamu kwa wote. Kumbukumbu hiyo  ni ukumbusho wa nguvu kwamba kutambua historia ni hatua ya lazima kuelekea jamii yenye haki na ujumuishi kwa vizazi vijavyo.”

Viongozi wa serikali wanahimizwa mshikamano wa kimataifa ili kujenga mustakabali wa usawa na haki za binadamu

Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa lihitimisha ujumbe wake kwa kusisitiza kuwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu yanathibitisha tena dhamira yao ya kupambana na ubaguzi wa rangi na kuhakikisha haki kwa wote. Hakusahau kusema  kuwa wakati dunia inapotafakari historia hii yenye uchungu, viongozi wanahimizwa mshikamano wa kimataifa katika kujenga mustakabali wa heshima, usawa, na haki za binadamu kwa wote. Kwa nia hiyo  alisema “kumbukumbu hii ni ukumbusho wa nguvu kwamba kutambua historia ni hatua ya lazima kuelekea jamii yenye haki na ujumuishi kwa vizazi vijavyo.”

27 Machi 2025, 16:19